Kiongozi Muadhamu: Tarehe 22 Bahman ya mwaka huu itakuwa yenye kuvutia
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, amyataja masiku ya Mwenyezi Mungu na minasaba ya matukio muhimu ya mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni ishara ya uimara na uthabiti wa mfumo, na kusisitiza kwamba, mwaka huu na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, tarehe 22 Bahman ya mwaka huu itakuwa yenye kuvutia.
Kiongozi Muadhamu Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo Alkhamisi inayosadifiana na siku ya kihistoria ya kutoa kiapo cha utiifu cha makamanda wa kikosi cha anga, yaani tarehe 19 Bahman 1357 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 8 Februari 1979 Miladia ambapo pia amekutana na makamanda na askari wa kikosi hicho cha anga. Amesema kuwa, mwaka huu na kutokana na miamala hasi ya baadhi ya viongozi wa Marekani na wasio wa Marekani, wananchi wa taifa hili wanahisi kwamba adui anafanya njama nyingi za kiaudui dhidi ya nchi yao na ni kwa ajili hiyo na kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, ushiriki wa wananchi katika maandamano ya tarehe 22 Bahman sawa na tarehe 11 Februari, utakuwa wa aina yake na wenye hamasa kubwa ambapo umati mkubwa wa wananchi utashiriki.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja mapinduzi ya Kiislamu kuwa uhakika wa uhai ambapo sambamba na kusisitiza kwamba, uimara na uthabiti wa mapinduzi hii leo ni zaidi ya siku za mwanzoni, amesema kuwa, wanamapinduzi wa leo wako imara na wenye uelewa wa hali ya juu na muono kuliko wanamapinduzi ya siku za mwanzoni na ni kwa msingi huo, ndio maana Mapinduzi ya Kiislamu yamezidi kukamilika na kufanikiwa kimaendeleo. Kadhalika Ayatullah Ali Khamenei amesema 'kusimama imara dhidi ya dhulma na kupinga ufisadi katika ngazi za kimataifa' ni miongoni mwa siasa kuu za Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kwamba, hii leo utawala wa kidhalimu na katili zaidi duniani, ni serikali ya Marekani ambayo ni mbaya kuliko hata kundi hatari la Daesh (ISIS). Akiashiria kwamba kundi la Daesh liliasisiwa na Marekani ambapo hata rais wa sasa wa Marekani Donald Trump alilikiri mara kadhaa suala hilo katika kampeni zake za uchaguzi, Kiongozi Muadhamu amesema kuwa, mbali na Washington kuanzisha kundi hilo hatari, imeendelea kuliunga mkono kwa misada, huku ikidai katika propaganda zake kimataifa kuwa ni muungaji mkono wa haki za binaadamu, wenye kudhulumiwa na haki za wanyama duniani.
Kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia masuala mbalimbali yakiwemo ya nchini Iran, eneo la Mashariki ya Kati na nje ya eneo. Sherehe za kumbukumbu ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran zitafika kileleni tarehe 22 Bahman sawa na tarehe 11 Februari mwaka huu ambapo mamilioni ya raia wa Jamhuri ya Kiislamu watafanya maandamano makubwa katika miji yoye ya nchi hii kutangaza uungaji mkono wao kwa mfumo wa Kiislamu nchini.