Iran yataka uchunguzi kuhusu jaribio la kushambulia nyumba ya balozi wake Vienna
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetaka uchunguzi wa haraka ufanyike kuhusu jaribio la kutekeleza hujuma kwa kutumia kisu katika makao ya balozi wake mjini Vienna, Austria.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi amesema aliyepanga kutekeleza hujuma hiyo alikuwa na umri wa miaka 26 na ana uraia wa Austria.
Vyombo vya habari vya Austria vinasema mtu aliyekusudia kutekeleza hujuma hiyo ya kisu alipigwa risasi na kuuawa na polisi Jumapili usiku nje ya makao ya balozi wa Iran mjini Vienna katika mtaa wa Heitzing wakati akijaribu kupita kizuizi cha mlinzi na kuingia katika jengo.
Msemaji wa Polisi ya Austria Harald Moeser amasema mshambuliaji huyo alikufa papo hapo baada ya mlinzi kumpiga risasi mara nne. Aliuawa baada ya gesi ya pilipili iliyotumiwa dhidi yake kushindwa kumzuia.
Hujuma hiyo imekuja masaa kadhaa baada ya balozi wa Iran mjini London Hamid Baeidinejad kusema amepokea ujumbe wa kutisha kumuaa kutoka kundi la wenye misimamo mikali la Shirazi ambalo lilihusika na hujuma dhidi ya ubalozi wa Iran mjini London.
Itakumbukwa kuwa Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini London adhuhuri ya Ijumaa ulishambuliwa na kundi moja la watu wanaojiita wafuasi wa kundi la mrengo wa Shirazi. Wavamizi hao walipanda katika ukuta wa ubalozi na kuiteremsha bendera ya Iran huku wakipeperusha bendera ya pote lao. Kwa mujibu wa Shirika Rasmi la Habari la Iran, IRNA, polisi ya Uingereza ilichukua muda mrefu kabla ya kuwakamata waliotekeleza hujuma hiyo.
Pote la Shirazi ambalo pia linatajwa kuwa ni "Mashia wenye kupata himaya ya Uingereza" linaongozwa na mtu anayejulikana kama Sadeq Shirazi. Hilo ni pote ambalo pia huyavunjia heshima matukufu ya Waislamu wa Ahlu Sunna.