Iran: Hatuna chuki na Saudia; iwapo itavamiwa, Tehran itakuwa ya kwanza kuihami
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwa bahati mbaya ikitokea Saudi Arabia ikabiliwe na uvamizi wa maajinabi au ugaidi, Tehran itakuwa ya kwanza kujitokeza kuihami na kuisaidia.
Mohammad Javad Zarif aliyasema hayo jana katika Kituo cha Mafunzo ya Kistrataji mjini Islamabad nchini Pakistan na kuongeza kuwa, Iran ina jukumu la kuhakikisha kuwa nchi jirani zake hazikabiliwi na vitisho vya aina yoyote.
Amesema, na hapa tunanukuu, "Tunaamini kuwa, usalama wa majirani zetu ni usalama wetu, na uthabiti miongoni mwa majirani zetu ni uthabiti kwa nchi yetu na eneo zima." Mwisho wa kunukuu.
Zarif amesema anatumai kuwa viongozi wa Saudia watakuwa na msimamo kama huu wa Iran kwa kuwadhaminia usalama jirani zake, na kwamba watakuwa tayari kwa ajili ya mazungumzo ya kuipatia ufumbuzi migogoro na tofauti zilizopo.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, tatizo la Riyadh ni kuitakidi kwamba ni kwa maslahi yake kuionyesha dunia kuwa Saudia inakabiliwa na tishio la kiusalama. Amebainisha kuwa, viongozi wa Riyadh wanatakiwa kufahamu kwamba, namna ambavyo Iran haiwezi kuindoa Saudia kwenye eneo hili la Mashariki ya Kati, ndivyo hivyo ambavyo Saudia haiwezi kuiondoa Iran katika eneo.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amesema daima Tehran imekuwa ikiinyooshea Saudia mkono wa muamana na muamala, likiwemo pendekezo la mazungumzo ya pande mbili lililotolewa na Nawaz Sharif, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan.