Zarif aanza safari ya kuzitembelea China, Russia na Brussels kuhusu JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i44410
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo Jumapili ameelekea mjini Beijing, katika safari ya kuzitembelea China, Russia na Ubelgiji; ziara yenye lengo la kutathmini utayarifu wa jamii ya kimataifa wa kuihakikishia Iran kuwa itasalia katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, licha ya Marekani kujiondoa kwenye mapatao hayo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 13, 2018 07:32 UTC
  • Zarif aanza safari ya kuzitembelea China, Russia na Brussels kuhusu JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo Jumapili ameelekea mjini Beijing, katika safari ya kuzitembelea China, Russia na Ubelgiji; ziara yenye lengo la kutathmini utayarifu wa jamii ya kimataifa wa kuihakikishia Iran kuwa itasalia katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, licha ya Marekani kujiondoa kwenye mapatao hayo.

Ziara hii inajiri chini ya wiki moja, baada ya Rais Donald Trump kutangaza kuiondoa Marekani kwenye mapatano hayo ya kimataifa, yaliyofikiwa Julai mwaka 2015 na kuanza kutekelezwa Januari mwaka 2016.

Baada ya kutoka Beijing, Mohammad Javad Zarif anatazamiwa kuitembelea Moscow na kisha Brussels, ambapo atakutana na mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, pamoja na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini.

Tayari EU imetoa radiamali hasi kuhusu uamuzi huo wa Trump wa kujitoa katika makubaliano ya JCPOA na kusisitiza kuwa  kuna udharura wa kuyalinda makubaliano hayo.

Dakta Javad Zarif nchini China

Kabla ya kuondoka nchini alfajiri ya leo, Zarif ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, "Utawala wenye misimamo ya kufurutu ada wa Trump umepuuza muafaka wa kimataifa uliotambuliwa kama ushindi wa kidiplomasia na jamii ya kimataifa. Iran ipo tayari kuanza tena kurutubisha urani kwa kiwango cha juu na bila mipaka yoyote, lakini itakuwa vinginevyo iwapo Ulaya italipa taifa hili dhamana ya kweli na ya kivitendo, kuwa itaendeleza uhusiano wa kibiashara na Iran licha ya vikwazo vipya vya Marekani."

Makubaliano hayo ya nyukilia yanayojulikana kama mpango kamili wa mapatano JCPOA yalifikiwa mwaka 2015 kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi kubwa duniani yaani, Russia, China, Uingereza, Ufaransa, Marekani na Umoja wa Ulaya.