Apr 07, 2016 16:20 UTC
  • Kerry aiomba Iran isaidie kuhatimisha vita Syria na Yemen

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry, ameomba msaada wa Iran ili kuhatimisha vita katika nchi za Syria na Yemen.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari mapema leo kabla ya mazungumzo yake na mawaziri wenzake wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi huko nchini Bahrain.

Iran "itusaidie ili tuhatimishe vita Yemen.... na Syria, ili (vita) visishadidi na itusaidie ili tuweze kubadilisha hali ya eneo hili", amesema Kerry.

Tangu mwezi Machi mwaka jana, kwa uongozi wa Saudi Arabia, nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi ukiondoa Oman, zimeanzisha mashambulio dhidi ya Yemen kwa lengo la kumrejesha madarakani Abd Rabbuh Mansour Hadi, Rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuidhoofisha harakati ya wananchi ya Ansarullah.

Wayemeni wapatao 9,400 wakiwemo wanawake na watoto 4,000 wameuliwa, na miundombinu ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu imeangamizwa kutokana na mashambulio hayo.

Baadhi ya nchi za Kiarabu zikiongozwa na Saudia pia zinaunga mkono makundi ya kigaidi nchini Syria kwa lengo la kumwondoa madarakani Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo.

John Kerry, ni kiongozi wa kwanza wa ngazi za juu wa Marekani kufanya safari nchini Bahrain tangu mwaka 2011 lilipoanza vuguvugu la mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala wa Aal Khalifa.

Marekani ni mmoja wa waungaji mkono wakuu wa utawala wa kifalme wa Bahrain ambao kwa msaada wa Saudia umekuwa ukitumia mkono wa chuma kukandamiza maandamano ya amani ya wananchi wa nchi hiyo ya kutaka mageuzi ya kisiasa.

Pamoja na hayo Kerry amewasifu watawala wa Bahrain kwa akile alichosema jitihada wanazofanya katika kuheshimu haki za binadamu.../

Tags