Rouhani: Nchi nyingi za dunia zimetangaza kutofuata sheria za ndani za Marekani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza kuwa, serikali ya Tehran imekuwa na mazungumzo mazuri na nchi mbalimbali za Ulaya, China, Russia, nchi jirani na mataifa muhimu ya Asia na akthari ya nchi hizo zimetangaza kwamba, hazifuati sheria za ndani za Marekani.
Rais Rouhani amesema hayo katika kikao cha leo cha Mihimili Mikuu Mitatu ya Dola yaani Serikali, Bunge na Idara ya Mahakama na kukosoa vikali siasa za maamuzi ya upande mmoja ya Marekani katika masuala mbalimbali.
Kikao cha Mihimili Mikuu Mitatu ya Dola kilifanyika leo kwa shabaha ya kujadili masuala muhimu ya sasa ya Iran kama ya uchumi na vikwazo visivyo halali vya serikali ya Marekani dhidi ya taifa hili.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Rais Hassan Rouhani ameashiria mwenendo wa ushirikiano wa kiuchumi wa Iran na matiafa mengine ya dunia na kueleza kuwa, ushirikiano huo utaendelea kama ilivyokuwa huko nyuma. Aidha amesema kuwa, njia ambayo Marekani iimeichagua pamoja na siasa zake kwa Iran, eneo la Mashariki ya Kati, Ulimwengu wa Kiislamu na hata kwa washirika wake si zenye kuendelea bali zitakwama.
Rais wa Iran ameashiria malalamiko na upinzani wa wananchi mjini London Uingereza dhidi ya safari ya Rais Donald Trump wa Marekani katika nchi hiyo ya Ulaya na kusisitiza kwamba, sera za watawala wa Marekani si za chokochoko na zisizo halali kwa taifa la Iran tu bali hata kwa mataifa mengine na hata kwa mataifa ambayo ni washirika wa Washington.