Siku ya mshikamano na watoto wa Palestina
Tarehe Tisa mwezi Mehr ambayo ni sawa na Okotoba Mosi 2018 imepewa jina la Siku ya Kuonyesha Mshikamano kwa Watoto na Vijana wa Kipalestina katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Hii ni nembo inayodhihirisha matakwa ya watoto wa Kiirani kwa mabeberu wa dunia na hatua yao ya kutangaza kuwa pamoja na kushikamana na watoto na vijana wa waliodhulimika wa Palestina. Tarehe Mosi Oktoba mwaka 2000 katika siku za mwanzo za mapambano ya Intifadha ya pili yaani (Intifadha ya al Aqsa); televisheni mbalimbali duniani zilionyesha picha ya kuuawa kinyama na askari katili wa Israel, Muhammad al Durrah kijana Mpalestina aliyekuwa na miaka 12 ambaye alikuwa amejificha ubavuni mwa baba yake ili kujinusuru na risasi za wanajeshi hao wa Kizayuni. Tukio hilo la kutisha lililorekodiwa na mpiga picha wa kanali ya pili ya televisheni ya Ufaransa na kisha kuonyeshwa na televisheni hiyo liliishia kwa kuuliwa shahidi mtoto huyo wa Kipalestina. Kijana huyo alipigwa risasi moja kichwani na wanajeshi walenga shabaha stadi wa utawala wa Kizayuni na kufa shahidi; na tukio hilo kuakisiwa pakubwa na vyombo vya habari duniani kote. Mauaji ambayo yalimfanya Muhammad al Durrah kuwa nembo ya muqawama na ya siku ya watoto wa Kipalestina wanaoua kinyama bila ya hatia.

Kwa mnasaba huo Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) imepasisha tarehe Tisa mwezi Mehr katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni Siku ya Kuonyesha Mshikamano kwa Watoto na Vijana wa Palestina. Kuhusiana na suala hili, shule kadhaa za jiji la Tehran jana zilipiga kengele katika kudhihirisha mshikamano wao kwa watoto wa Kipalestina. Marasimu hayo ya kimaonyesho yalifanyika kwa uungaji mkono wa Taasisi ya Kuwatetea Wananchi wa Palestina na kuhudhuriwa na wanaharakati wa masuala ya Palestina na wawakilishi wa vyombo vya habari.
Hakuna shaka kuwa Mapinduzi ya Kiislamu na vijana wa Kiirani wamekuwa na nafasi muhimu katika kuhuisha kadhia ya Palestina na mwamko wa Ulimwengu wa Kiislamu na kuchukuliwa hatua katika uga wa kimataifa kuhusu suala la Palestina na masaibu yanayowakumba raia wa taifa hilo. Hapa tunatupia jicho hali ya kusikitisha na ya maafa inayowasibu Wapalestina ikiwa ni natija ya hatua za ukandamizaji na kupenda kujitanua za utawala wa Kizayuni.
Utawala wa Kizayuni unatekeleza siasa zake za kibaguzi ili kukiangamiza kizazi cha Wapalestina na wakati huo huo umeziweka katika ajenda yake ya kazi siasa za kuuawa watoto wa Kipalestina. Watoto wa Kipalestina ni wahanga wakuu wa jinai za kivita na mauaji ya kizazi yanayofanywa na utawala wa Israel katika ardhi za Palestina inazozikalia kwa mabavu tangu uanze kughusubu ardhi za Palestina mwaka 1948. Hii ni katika hali ambayo watoto wa Kipalestina kila uchao wanaendelea kukabiliwa na jinai za utawala huo wa Kizayuni. Wakati huo huo ikiwa ni katika kutekeleza siasa za undumakuwili mkabala na kuufumbia macho utawala wa Kizayuni, Umoja wa Mataifa hadi sasa umekwepa kuuweka utawala huo katika orodha ya serikali zinazokiuka haki za watoto licha ya matakwa makubwa ya jamii ya kimataifa. Mauaji yanayofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina kukiwemo kuwaua watoto ni mfano wa wazi wa jinai dhidi ya ubinadamu, maangamizi ya kizazi; na kukiri taasisi mbalimbali za Umoja wa Mataifa kunathibitisha jambo hilo. Aidha kuendelea kuuliwa watoto wa Kipalestina kulipelekea utawala huo unaotenda jinai kupachikwa jina la "utawala unaoua watoto" wakati wa vita vya siku 22 huko Ghaza.

Si hayo tu bali kushindwa Umoja wa Mataifa kuuchukulia hatua utawala huo ghasibu, ambapo ripoti za wawakilishi na taasisi mbalimbali za umoja huo zimekiri kuhusu mauaji ya watoto yanayofanywa na utawala huo, na wakati huohuo kushindwa kuuweka utawala huo katika faharasa ya serikali zinazoua watoto; kumeutia kiburi utawala huo cha kuzidisha kila aina ya jinai dhidi ya watoto wa Kipalestina bila ya kuwa na wasiwasi wowote wa kukabiliwa na mkondo wa sheria.