Rais Rouhani ayashukuru majeshi ya Iran kwa jibu kali kwa magaidi + Video
Rais Hassan Rouhani amevishukuru vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa majibu makali na ya kina dhidi ya viongozi wa magaidi waliohusika katika shambulizi la kigaidi la Ahvaz, kusini magharibi mwa Iran na kusisitiza kuwa: Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limetoa majibu makali kabisa kwa magaidi ambao waliwashambulia bila huruma wanawake na watoto wadogo nchini Iran.
Rais Hassan Rouhani alisema hayo jana (Jumatano) mbele ya baraza lake la mawaziri na huku akiwatahadharisha maadui kuwa daima majibu ya Iran yatakuwa makali na yenye madhara makubwa amesema, kama ambavyo Iran imetoa jibu kali kwa watekelezaji wa shambulizi hilo la kigaidi, ni hivyo hivyo inawahesabu walioamrisha na kupanga ugaidi huo kuwa nao wanastahki majibu sawa na waliyopata watekelezaji wa shambulizi hilo.
Rais Rouhani amezungumzia pia njama za Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa, hivi sasa Marekani imetengwa kimataifa na hakuna mtu anayeweza kukubaliana na ubeberu wa Marekani.
Amesema lengo la viongozi wa Marekani la kuishinikiza Iran ni la ndani ya Marekani kwenyewe na halina uhusiano wowote na eneo hili la Mashariki ya Kati na wala dunia na Waarabu ambao imewapora fedha zao zote.
Ameongeza kuwa, juhudi zote za Marekani zinalenga kuishinikiza Iran ifanye nayo mazungumzo hata ya daraja la chini kabisa na baadaye iwatangazie walimwengu kuwa vikwazo vyake dhidi ya Iran vimefanikiwa.
Rais Rouhani pia amesema, taifa la Iran limesimama imara kupambana na vikwazo vya Wamarekani kwani wananchi wa Iran ni wananchi wanamuqawama, mashujaa na wanaoelewa vyema mambo na kamwe hawatotetereka mbele ya njama za Marekani.