Oct 31, 2018 15:52 UTC
  • Rais Rouhani: Marekani itafeli tu katika njama zake mpya dhidi ya Iran

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, licha ya kuwepo vikwazo vya Marekani dhidi ya Tehran, lakini nchi nyingi duniani za Asia na Ulaya zina hamu ya kuendeleza ushirikiano wao na Iran.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo na kuongeza kuwa, Wamarekani watashindwa tu katika njama zao mpya na wataanza kulegeza kamba na kurudi nyuma pole pole kwani ni jambo lililo wazi kuwa kamwe hawatoweza kuufikisha kwenye sifuri uuzaji nje wa mafuta ya Iran.

Rais Rouhani aidha amesema, pamoja na kwamba Wamarekani wanajribu kuwatia hasira wananchi wa Iran kutokana na mashinikizo yao ya kisaikolojia na kiuchumi, lakini wananchi wa Iran tangu zamani wana hasira kubwa dhidi ya Wamarekani kutokana na jinai zao dhidi ya taifa hili.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema, sisi tunaweza kuvishinda kiurahisi sana vikwazo vya Marekani na tunapenda kuzieleza pande zinazofanya nasi biashara kwamba, vikwazo vya Marekani ni vya kupita tu lakini ushirikiano wetu na wao ni wa kudumu.

Vile vile ameishukuru serikali na wananchi wa Iraq kwa mapokezi mazuri mno waliyowapa wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW waliomiminika nchini humo kwa ajili ya Arubaini ya Imam Husain AS na kusema kuwa, ujumbe wa Arubaini ya Husain ni ujumbe wa ukombozi, uhuru, usalama na amani kwa dunia nzima, hivyo wapenzi wote wa ukombozi na ubinadamu wanapaswa kufuata njia hiyo ya Imam Husain AS.

Tags