Kharrazi: Wananchi wa Iran wamesimama kidete dhidi ya mashinikizo ya Marekani
-
Dakta Kamal Kharrazi
Mkuu wa Baraza la Stratejia za Uhusiano wa Nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, licha ya kuweko matatizo hapa nchini yanayotokana na vikwazo vya Marekani, lakini wananchi wa Iran wako pamoja na wamesimama kidete kwa ajili ya kukabiliana na mashinikizo ya Washington.
Dakta Kamal Kharrazi amesema hayo katika mkutano na shakhsia na watu wenye vipaji vya kisiasa wa Austria huko Vienna ambapo akitoa tathmini yake kuhusiana na masuala ya Mashariki ya Kati na uhusiano wa Iran na Ulaya amesema kuwa, taifa la Iran litafanikiwa kuyashinda matatizo na vikwazo vya Marekani kwa kutegemea rasilimali za ndani, msaada wa nchi rafiki pamoja na ubunifu wa nchi za Ulaya.
Mkuu wa Baraza la Stratejia za Uhusiano wa Nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema wananchi wa Iran hawatasalimu amri mbele ya njama za Marekani na kutokana na moyo na irada waliyonayo ya kukabiliana na njama za adui dhidi ya taifa lao watafanikiwa kuvuka salama na kumshinda adui.

Tarehe 5 Novemba Marekani ilianza kutekeleza awamu nyingine ya vikwazo vyake vya kidhalimu dhidi ya Iran ambavyo vinajumuisha sekta ya benki, mabadilishano ya kifedha na uuzaji wa mafuta ya Iran.
Hata hivyo baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani, Rais Donald Trump alisema kuwa amefumbia jicho kuiwekea Iran vikwazo kamili vya mafuta ili kuzuia kuvurugika kwa bei ya mafuta.
Tangazo hilo la Trump limetathminiwa kama pigo kwake na kulegeza msimamo wake wa awali wa kuiwekea vikwazo vikali Iran hususan sekta yake ya mafuta na kuzuia kuuzwa hata pipa moja la mafuta ya Iran.