Iran yaikosoa Ulaya kwa kuchelewa kutekeleza mfumo wa kifedha wa SPV
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50668-iran_yaikosoa_ulaya_kwa_kuchelewa_kutekeleza_mfumo_wa_kifedha_wa_spv
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameukosoa Umoja wa Ulaya kwa kuchelewesha utekelezwaji wa mfumo mpya wa kifedha baina ya Iran na umoja huo unaojulikana kama SPV.
(last modified 2026-04-23T06:05:17+00:00 )
Jan 05, 2019 23:10 UTC
  • Iran yaikosoa Ulaya kwa kuchelewa kutekeleza mfumo wa kifedha wa SPV

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameukosoa Umoja wa Ulaya kwa kuchelewesha utekelezwaji wa mfumo mpya wa kifedha baina ya Iran na umoja huo unaojulikana kama SPV.

Ikumbukwe kuwa baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran, JCPOA, mwezi Mei mwaka jana, ulianzishwa mchakato wa kubuni Mfumo Maalumu kwa Ajili ya Mabadilishano ya Kifedha na Iran, kwa Kiingereza Special Purpose Vehicle,(SPV).

Bahram Qassemi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran katika mahojiano yake na shirika la habari la IRIB ameashiria kuzembea nchi za Ulaya katika kuanzisha mfumo huo na kutahadahrisha kuwa subira ya Iran ina kikomo.

Ameongeza kuwa, nchi za Umoja wa Ulaya zimekumbwa na udhaifu mkubwa katika utekelezaji wa SPV na kuongeza kuwa, nchi za Ulaya ndizo zitakazobeba dhima ya kutotekelezwa mfumo huo wa kifedha.

Qassemi amesema kuwa Iran imetekeleza majukumu yake yote katika mapatano ya JCPOA na kuongeza kuwa: "Nchi za Ulaya zinapaswa kuwa na misimamo huru ya kiuchumi na zisiwe tegemezi kwa Marekani." Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia ameashiria matamshi dhidi ya Iran yaliyotolewa na Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuwa eti vikwazo dhidi ya Iran ni kwa maslahi ya Wairani na kusema dhana kama hivyo ni ghalati kabisa.

Kuhusu shughuli za makombora ya kujihami ya Iran, Qassemi amesema sera za Iran kuhusu makombora zimejengeka katika msingi wa kujihami na kuzuia adui na si kinyume cha azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Aidha amesema Marekani imepata madhara kutokana na sera zake duniani.