Jan 10, 2019 16:03 UTC
  • Rais Rouhani: Tunajifakharisha kwa makombora yetu ya kiulinzi na kielimu

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, makombora leo hii ni zana ya kujilinda Iran na taifa letu leo hii linajivunia na linaona fakhari kubwa kuwa na nguvu za kiulinzi za makombora.

Rais Rouhani amesema hayo leo katika kumbukumbu za mwaka mmoja wa kifo cha Ayatullah Hashemi Rafsanjani, mkuu wa zamani wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Rais Rouhani ameongeza kuwa, katika wiki chache zijazo, Iran itarusha katika anga za mbali satalaiti mpya kwa kutumia makombora yaliyotengenezwa na wataalamu wetu wenyewe.

Amesema, taifa la Iran limefanya kazi kubwa kwa kufikia mapatano ya nyuklia ya JCPOA kiasi kwamba katika kipindi cha siku moja, mapatano hayo yalifuta maazimio sita ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaliyokuwa dhidi ya Iran.

Marhum Ayatullah Hashemi Rafsanjani

 

Vile vile amesema, lengo kuu la vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Iran lilikuwa ni kuangamiza fursa ya kimataifa ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Aidha amezungumzia nguvu za kiulinzi na kiteknolojia za sasa hivi za Iran na kusema, adui ametumia nguvu zake zote kuiwekea mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi Iran, lakini ni jambo lisilo na shaka hata chembe kwamba njia ya Mapinduzi ya Kiislamu itaweza kulindwa kupitia umoja, mshikamano na uvumilivu.

Ayatullah Hashemi Rafsanjani alifariki dunia hapa mjini Tehran tarehe nane Januari 2017 kutokana na mardhi ya moyo.

Tags