Apr 16, 2016 16:06 UTC
  • Rouhani: Iran itaendelea kuwa pamoja na OIC

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Tehran itaendelea kuwa pamoja na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) maadamu jumuiya hiyo inashikamana na malengo yake ya asili.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo mjini Istanbul katika kikao cha waandishi habari akiwa na mwenyeji wake wa Uturuki, Rais Recep Tayyip Erdogan. Amesema kuwa malengo makuu ya Jumuiya ya Ushirkiano wa Kiislamu ni kuimarisha umoja wa jamii za Waislamu na kutetea malengo ya Wapalestina.

Kuhusu uhusiano wa Tehran na Ankara, Rais Rouhani amesema kwa sasa kuna hali nzuri ya kuimarisha ushirikiano wa pande hizo mbili. Ameongeza kuwa, benki na masoko ya hisa ya nchi hizo mbili yanaweza kushirikiana na kuleta mabadiliko.

Vilevile ameashiria hali inayotia wasiwasi ya Yemen na Iraq na kusema: Kuna udharura wa kusaidiwa watu wa nchi hizo kwa ajili ya kurejesha amani katika nchi zao kwa sababu suala hilo lina maslahi pia kwa nchi nyingine. Ametilia mkazo udharura wa kusitishwa vita na mapigano na kukabiliana na ugaidi wa aina zote.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekwenda Uturuki kushiriki mkutano wa viongozi wa nchi wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

Tags