Uwezo mkubwa wa kijeshi wa Iran umemzuia adui kushambulia
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema: "Uwezo mkubwa wa kujihami na kuhujumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni jambo ambalo limemfanya adui asithubutu kutekeleza hujuma yoyote ya kijeshi dhidi ya nchi hii."
Brigedia Jenerali Amir Hatami, Waziri wa Ulinzi wa Iran ameyasema hayo Jumamosi na kuongeza kuwa: "Kuimarishwa uwezo wa kijeshi na kujihami wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni moja kati ya mihimili muhimu zaidi ya stratijia ya kijeshi katika kukabiliana na vitisho." Ameongeza kuwa, madola ya kibeberu yanaipinga Iran kwa sababu mfumo wa kisiasa wa Iran, yaani Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni mfumo unaopinga ubeberu na utegemezi.
Brigedia Jenerali Amir Hatami ameashiria hujuma ya makundi ya kigaidi kama vile Daesh au ISISI nchini Syria na Iraq na kusema: "Wamagharibi na hasa Wamarekani na waitifaki wao katika eneo ambao wanaunga mkono ISIS hawakuwa wakidhani kwa uungaji mkono wao mkubwa waliokuwa wamewapa magaidi, ingekuwa rahisi kuangamizwa na kusambaratishwa magaidi hao watenda jinai."
Waziri wa Ulinzi wa Iran ameendelea kusema kuwa, Marekani na waitifaki wake walianzisha ISIS kwa lengo la kubuni donda jingine la saratani katika kitovu cha nchi za Kiislamu ambalo lingeshabihiana na utawala utendao jinai wa Kizayuni. Amesema kila njama itasambaratika kutokana na nafasi muhimu ya Iran kukabiliana na njama hizo.
Brigedia Jenerali Hatami amesema maadui wa Iran na hasa Marekani na utawala wa Kizayuni wanatoa tuhuma na kueneza propaganda dhidi ya Iran baada ya kila tukio katika eneo, na mfano wake ni tukio la Bandari ya Al Fujairah nchini Imarati. Amesema maslahi ya adui yako katika kuibua machafuko na ukosefu wa usalama katika eneo sambamba na kueneza chuki dhidi ya Iran, kuuza silaha na kupora utajiri wa eneo na hatimaye kupelekea kadhia ya Palestina isahaulike.