Ugaidi wa kiuchumi wa Marekani; Iran haitasalimu amri
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, sera za vikwazo za serikali ya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran ni ugaidi; na akasisitiza kwamba: Iran haitafanya mazungumzo na magaidi.
Mohammad Javad Zarif alitoa kauli hiyo jana mbele ya waandishi wa habari mjini New York, makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Dakta Zarif amesema, vita vya kiuchumi vya Marekani haviwalengi wanajeshi au viongozi wa Iran, bali vinawalenga raia wa kawaida wa taifa hili; na akafafanua kwa kusema: Hii ni hatua ya kigaidi, kwa sababu ugaidi huwa unawalenga raia ili kufanikisha mpango wake wa kisiasa.
Vikwazo na mashinikizo ni sera ambayo Marekani imekuwa ikiitumia kila mara dhidi ya taifa la Iran tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Baada ya mapinduzi hayo kupata ushindi na kudhihiri utambulisho halisi wa Kiiran na moyo wa kujitawala wa taifa hili, maslahi haramu ya Marekani yalitoweka moja kwa moja nchini Iran. Na hiyo ndiyo sababu iliyozifanya serikali tofauti zilizoingia madarakani nchini Marekani ziamue kutumia silaha ya vikwazo na njama mbali mbali ili kujaribu kubadilisha siasa za taifa na serikali ya Iran.
Akiizungumzia nukta hiyo, Kazem Gharib Abadi, mwakilishi wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao mjini Vienna, Austria amesema, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na akafafanua kwamba: Marekani iko mstari wa mbele katika uchukuaji hatua za ukiukaji sheria na inavitumia vikwazo kama wenzo wa kubadilisha siasa na sera za nchi zingine.
Idris Jazayeri, ripota maalumu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, yeye pia amekosoa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran akisema, vikwazo hivyo ni mzingiro ulio kinyume na sheria na kisasi dhidi ya halaiki, ambapo yote mawili yanakinzana na sheria za kimataifa za kibindamu.
Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, taifa la Iran limekuwa likipiga hatua kuelekea ustawi na maendeleo kwa kutegemea utambulisho wake wa Kiirani na uwezo wake lenyewe, ambapo leo hii Iran imeweza kupata mafanikio makubwa katika nyuga nyingi.
Mafanikio iliyopata Iran, ambayo ni matunda ya muqawama na kusimama kwake imara katika kukabiliana na maadui, yamekuwa ni sera na mfano uliokubalika na kuigwa na mataifa yenye fikra huru duniani; na hicho ndicho chanzo cha uhasama na uadui wa Marekani dhidi ya taifa la Iran.
Msimamo wa kujitawala na kuwa huru katika kujiamulia mambo yake pamoja na kujivua na utegemezi kwa madola ya kibeberu ndio manifesto ya Mapinduzi ya Kiislamu, ambayo baada ya miaka 40 ya kujivunia, sasa yameingia kwenye muongo wake wa tano.
Kadiri taifa la Iran lilivyopiga hatua moja mbele kuelekea kwenye ustawi na mafanikio, kwa kiwango hicho hicho Marekani nayo imekuwa ikiliwekea vikwazo taifa hili; hata hivyo usuli na misingi mikuu ya Iran inayotokana na Mapinduzi ya Kiislamu bado haijabadilika.
Tajiriba ya miaka 40 ya kusimama imara taifa la Iran imethibitisha kwa uwazi kabisa kwamba, vyovyote itakavyokuwa, taifa hili halitasalimu amri kwa viongozi wa serikali ya Marekani; hata kama serikali kama ya Donald Trump itatumia ugaidi wa kiuchumi kukabiliana na wananchi wa Iran.
Wakati rais huyo wa Marekani ameamua kutumia "vitisho" na "mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa" ili kuiburuza Iran ikubali kufanya mazungumzo, Jamhuri ya Kiislamu imetumia "Muqawama wa kiwango cha juu kabisa" ambao umeisambaratisha sera hiyo ya serikali ya Washington.
Japokuwa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya taifa la Iran, na ambavyo vinaendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, ndivyo vikwazo vikali zaidi kuwahi kuwekewa taifa hili, lakini Washington inapaswa ifahamu kuwa sera hizo za vikwazo hazitaweza katu kuipigisha magoti Iran; na wala kutumia ugaidi wa kiuchumi hakutawawezesha wakaazi wa sasa wa White House kufanikisha ndoto ya alinacha wanayoota kuhusiana na serikali na wananchi wa Iran.
Ni kama alivyosisitiza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, kwamba: Taifa la Iran limedhulumika kutokana na vikwazo hivyo vya kidhalimu; lakini pamoja na hayo haliko dhaifu, bali liko imara na lenye nguvu. Na kwa rehma za Mwenyezi Mungu, litaweza kwa nguvu na uwezo kamili kuyafikia makusudio na malengo yake yote liliyojiwekea.../