Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman zasisitiza kuimarisha ushirikiano baina yao
Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman leo wamekutana hapa mjini Tehran ambapo pamoja na mambo mengine wamesisitiza juu ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili.
Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na mgeni wake Yusuf bin Alawi wamesisitiza katika mazungumzo yao juu ya kudumisha mazungumzo na ushirikiano wa pande mbili.
Aidha Yusuf bin Alawi bin Abdullah na Dakta Muhammad Javad Zarif wamezungumzia matukio ya hivi karibuni katika eneo la Mashariki ya Kati na ya kimataifa kwa ujumla.
Kadhalika Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman sambamba na kuashiria katika mazungumzo yao juu ya uhusiano mzuri uliopo baina ya Tehran na Muscat wamesema kuwa, kuna haja ya kuendelezwa mazungumzo hayo na kubadilishana mawazo kuhusiana na matukio mbalimbali ya kieneo na kimataifa.
Hii ni safari ya pili ya Yusuf bin Alawi bin Abdullah, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Oman hapa mjini Tehran katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Yusuf bin Alawi anakuwa kiongozi wa pili wa ngazi za juu wa eneo hili la Mashariki ya Kati kuitembelea Iran katika kipindi cha siku chache zilizopita, ambapo juma lililopita, Adil Abdul-Mahdi, Waziri Mkuu wa Iraq alifanya safari hapa nchini na kukutana na viongozi mbalimbali wa taifa hili.