Zarif amwambia Pompeo: Kipindi cha "madola makubwa" kimepita
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemwambia wenzake wa Marekani kwamba kipindi cha madola makubwa kimepita muda mrefu huko nyuma.
Muhammad Javad Zarif amesema katika ujumbe wake wa Twitter ulioandamana na matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo aliyotoa tarehe 4 Aprili akisema kuwa kuna udharura wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kukabiliana na madola makubwa matatu yaani Iran, Russia na China, kwamba: Marekani imeendelea kuiwekea vikwazo zaidi Russia ikiendeleza ugaidi wake sugu wa kiuchumi.
Dakta Zarif amesema, ni wazi kuwa wasiwasi wa Pompeo kuhusu "madola makubwa" sasa unageuka na kuwa woga na wahka.
Katika ujumbe wake mwingine alioutoa mapema jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliitaka Marekani ikomeshe mwenendo wa kujitenga na kuongeza kuwa: Nguvu na biashara ya kimataifa imo katika mabadiliko na uhakika huo hautabadilishwa na ugaidi wa kiuchumi dhidi ya Iran na China au kujiondoa Marekani katika mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF).
Jana Ijumaa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo alitangaza habari ya kujiondoa rasmi nchi hiyo katika mkataba wa Kuzuia Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati kwa kifupi INF.
Russia ilijibu mapigo kwa kujikujitoa rasmi kwenye makubaliano ya INF baada ya hatua iliyochukuliwa na Marekani.
Makubaliano hayo ya pande mbili ya kutokomeza Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF) yalisainiwa mwaka 1987 na viongozi wa wakati huo wa Marekani na Shirikisho la Kisovieti la Urusi ya zamani na kutajwa kama hatua muhimu ya kuondoa hali ya mivutano katika enzi hizo za Vita Baridi.
Makubaliano ya INF yalipiga marufuku Washington na Moscow kuweka makombora yao ya Balestiki na Cruise barani Ulaya.