Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akutana na Rais wa Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55562-waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_iran_akutana_na_rais_wa_ufaransa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ijumaa amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Ufaransa mjini Paris.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 24, 2019 02:58 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akutana na Rais wa Ufaransa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ijumaa amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Ufaransa mjini Paris.

Akijibu maswali ya waandishi habari baada ya kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema mkutano wake na Rais Emanuel Macron wa Ufaransa ulikuwa mzuri na kuongeza kuwa: "Mazungumzo  hayo ni muendelezo wa yale yaliyojadiliwa kwa njia ya simu baina ya marais wa nchi mbili wiki kadhaa zilizopita.

Zarif ameongeza kuwa katika mazungumzo yake na Macron wamepeana mapendekezo kuhusu njia za kutekeleza mapatano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kubainisha kuwa, Umoja wa Ulaya unapaswa kutekeleza ahadi ulizotoa kuhusu mapatano ya JCPOA kufuatia hatua ya upande mmoja ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa.

Zarif aliwasili Paris Alhamisi baada ya kumaliza safari yake mjini Oslo nchini Norway na kabla ya hapo alikuwa amezitembelea Sweden na Finland.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua hatua za kupunguza utekelezaji wa majukumu yake katika JCPOA  baada ya pande zingine katika mapatano hayo kutotekeleza ahadi zao. Tehran imesema iwapo pande zingine katika JCPOA zitatekeleza ahadi zao, basi nayo pia itarejea haraka katika utekelezaji wa ahadi zake kikamilifu.

Moja ya ahadi ambazo nchi za Ulaya zilikuwa zimesema zitatekeleza baada ya Marekani kujiondoa katika JCPOA kinyume cha sheria, ni kuanzisha mfumo wa mabadilishano ya kifedha maarufu kama INSTEX lakini bado madola ya Ulaya hayajatekeleza ahadi hiyo.