Zarif: Iran itatetea na kulinda maslahi yake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55627-zarif_iran_itatetea_na_kulinda_maslahi_yake
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaki kuingia vitani lakini italinda na kutetea maslahi yake.
(last modified 2025-11-30T06:27:20+00:00 )
Aug 27, 2019 07:49 UTC
  • Zarif: Iran itatetea na kulinda maslahi yake

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaki kuingia vitani lakini italinda na kutetea maslahi yake.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mahojiano na gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung, ambayo yamechapishwa katika toleo la leo la gazeti hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria kujitoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kueleza kwamba: Kwa mujibu wa ripoti 15 za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Iran imetekeleza ahadi na majukumu yake katika JCPOA, lakini pande zingine hazijafanya hivyo.

Amefafanua kuwa, kwa mujibu wa JCPOA jamii ya kimataifa na hasa wanachama wa makubaliano hayo wana wajibu wa kuhakikisha uhusiano wa kiuchumi wa Iran na nchi zote unarejea katika hali ya kawaida.

Kuhusu hatua ya Iran ya kupunguza kiwango cha uwajibikaji wake katika makubaliano hayo ya nyuklia, Dakta Zarif amesema, ikiwa usafirishaji mafuta ghafi ya Iran utaanza tena, Tehran itatekeleza tena majukumu yake katika JCPOA.

Baada ya hatua ya upande mmoja na ya kuhalifu sheria iliyochukuliwa na Marekani mnamo mwezi Mei 2018 ya kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Iran ilitekeleza kwa muda wa mwaka mzima kile ilichokiita "subira ya kistratejia" na kutoa muhula kwa pande zingine hususan nchi za Ulaya kutekeleza ahadi zao za kufidia kujitoa Marekani kwenye makubaliano hayo.

Kutokana na kushindwa kufanya hivyo, kuanzia Mei 8 mwaka huu, Iran ilianza kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA kulingana na vifungu vya 26 na 36 vya makubaliano hayo.

Baada ya awamu mbili za utekelezaji wa hatua hizo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonya kuwa itatekeleza awamu ya tatu na kali zaidi ya kupunguza uwajibikaji huo, endapo upande wa Ulaya hautatekeleza ahadi na majukumu yake kulingana na muhula mwengine uliopewa.../