Vaezi: Ujumbe wa masuala ya uchumi wa Iran kuelekea Ufaransa wiki ijayo
Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa ujumbe wa kiuchumi wa Iran wiki ijayo utafanya safari nchini Ufaransa.
Akizunguumza na vyombo vya habari leo mjini Tehran, Mahmoud Vaezi ameashiria maendeleo yaliyopatikana katika mazungumzo ya Iran na Ufaransa na kueleza kuwa: Wiki ijayo ujumbe wa kiuchumi wa Tehran utaondoka hapa nchini na kuelekea Ufaransa ili kujadiliana zaidi juu ya mazungumzo hayo.
Vaezi ameongeza kuwa Tehran itatangaza uamuzi wake kuhusu suala la kuchukua hatua ya tatu ya kupunguza utekelezaji wa majukumu yake ndani ya makubaliano ya JCPOA baada ya ujumbe huo wa kiuchumi wa Iran kurejea nchini.
Iran iliamua kufanya "subira ya kistratejia" ya mwaka mmoja baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano hayo ya nyuklia na imetoa muhula kwa pande shiriki katika makubaliano hayo ya JCPOA hususan nchi za Ulaya ambazo ziliahidi kufidia nakisi ya kujitoa huko kwa Marekani katika makubaliano hayo ya nyuklia ya kimataifa, kutekeleza majukumu yao.
Tarehe 8 mwezi Mei mwaka huu baada ya kuthibitika kwamba mipango yote ya Ulaya kwa ajili ya kufidia taathira za kiuchumi za kujitoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA imefeli, Iran ilitangaza kuwa inasitisha utekelezaji wa sehemu ya majukumu yake ndani ya JCPOA kwa mujibu wa vipengee vya 26 na 36 vya makubaliano hayo ya kimataifa.
Iran ilitoa muda wa siku 60 kwa pande zilizosalia katika makubaliano hayo ili zitekeleza majukumu yao hususan katika masuala ya kibenki na biashara ya mafuta. Tarehe 7 mwezi Julai mwaka huu baada ya kumalizika muhula huo wa siku 60 kwa nchi za Ulaya, Iran ilianza mchakato wa kurutubisha urani uliopita kiwango cha asiliia 3.67. Si hayo tu, bali Iran imezitahadharisha nchi za Ulaya kwamba itachukua hatua ya tatu iwapo nchi hizo hazitatekeleza majukumu yao kuhusu makubabaliano hayo ya nyuklia.