Zarif aikosoa Ulaya kwa kufuata mdundo wa ngoma ya Trump
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali nchi za Ulaya hususan Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ambazo zilisaini makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, kwa kushangilia madai na kauli zisizo na msingi zinazotolewa na Marekani dhidi ya Iran.
Mohammad Javad Zarif amezishangaa nchi hizo za Ulaya kwa kukubali mashinikizo ya Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa, "Ukiziona nchi za Ulaya hivi sasa zinajisogeza zaidi kwa Marekani, si kwa kuwa zimeona udhaifu na mapungufu kwetu (Iran), bali ni kwa kuwa zimeshindwa kuistahamili Washington."
Zarif alisema hayo jana usiku mjini Frankfort katika mazungumzo yake na raia wa Iran wanaoishi nchini Ujerumani. Zarif alipitia Ujerumani akiwa njiani kurejea hapa nchini, akitokea New York ailikoenda kushiriki mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amebainisha kuwa, "Katika kipindi cha miezi mitano iliyopita, nchi za Ulaya zimekuwa zikijaribu kufanya miamala ya kibashara na Iran, lakini hilo limeshindikana kwa kuwa bwana wao (Marekani) hajawapa kibali."
Tarehe 31 Januari mwaka huu, Umoja wa Ulaya na baada ya miezi kadhaa ya majadiliano na Tehran, hatimaye ulianzisha mfumo maalumu wa kibiashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliopewa jina la INSTEX ingawa tangu wakati huo EU imekuwa ikichelewesha utekelezwaji wa mfumo huo kwa visingizio mbalimbali.
Siku chache zilizopita, Waziri wa Fedha wa Marekani, Steven Mnuchin alisema kuwa viongozi wa nchi za Ulaya wameihakikishia Washington kwamba hawatochukua hatua yoyote ya kuvikwepa vikwazo ambavyo nchi hiyo imeiwekea Iran bila kushauriana na serikali ya Donald Trump.
Chini ya mashinikizo ya Marekani, viongozi wa nchi za EU wamesema iwapo Iran itachukua hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake kwenye makubaliano hayo mwezi Novemba mwaka huu, basi nchi hizo za Ulaya zitaanza kujiondoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.