Salami: Adui hana ujasiri wa kufyatua risasi hewa dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56402-salami_adui_hana_ujasiri_wa_kufyatua_risasi_hewa_dhidi_ya_iran
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema adui wa taifa hili hana uthubutu wala ujasiri wa kufyatua hata risasi moja hewa ndani ya mipaka ya nchi hii.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 03, 2019 22:10 UTC
  • Salami: Adui hana ujasiri wa kufyatua risasi hewa dhidi ya Iran

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema adui wa taifa hili hana uthubutu wala ujasiri wa kufyatua hata risasi moja hewa ndani ya mipaka ya nchi hii.

Meja Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa IRGC aliyasema hayo jana Alkhamisi katika marasimu ya kuwaenzi Mashahidi katika mji wa Arak, makao makuu ya mkoa wa Markazi na kusisitiza kuwa, njama za maadui za kuusambaratisha Mfumo wa Kiislamu hapa nchini hii leo zimevurugika kwa kiasi kikubwa kuliko wakati mwingine wowote ule.

Amebainisha kuwa, kutokana na maadui wa taifa hili kukosa irada na ujasiri wa kuishambulia kijeshi Iran ya Kiislamu, hivi sasa wanalenga uchumi, utamaduni na moyo wa Wairani. Amesema maadui pia wanahujumua sekta za usalama na sayansi za taifa hili, na ndiyo maana wameua shahidi wanasayansi kadhaa wa Iran.

Meja Jenerali Hussein Salami ameeleza bayana kuwa, miongozo ya busara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kufika katika upeo wa juu sekta ya sayansi na teknolojia hapa nchini, ni katika mambo yanayowalazimisha maadui wapange upya mahesabu na njama zao dhidi ya Iran.

Iran imezindua mafanikio mapya katika uga wa usalama

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, "Watoto wa Mapinduzi" wamesimama kidete ardhini, angani na baharini.

Ameeleza kuwa, "Waliodhani kuwa Iran itasalimu amri mbele ya maadui wamefeli. Wamarekani na Wazayuni hawawezi kushusha pumzi zao ndani ya ardhi ya Iran kwa kuwa tumewazibia nyufa zote."