Nov 03, 2019 08:01 UTC
  • Larijani: Trump ni nembo ya sura ya kuogofya ya Marekani

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema tabia ya Donald Trump ya kufichua sera haribifu zilizofichika za Ikulu ya White House ya Marekani imeweka hadharani sura halisi, mbaya na ya kuogofya ya Washington.

Ali Larijani amesema hayo leo Jumapili katika kikao cha Bunge hapa Tehran na kufafanua kuwa, "kwa bahati nzuri, Marekani hii leo ina rais ambaye anafanya kazi ya kila mtu, kwa kufichua sura halisi na ya kutisha ya sera za White House."

Larijani ameashiria kauli ya Trump akizungumza hivi karibuni kuhusu kuuawa kinara wa kundi la kigaidi la Daesh, Abu Bakr Baghdadi aliposema kuwa Marekani ipo Syria kwa ajili ya mafuta pekee, ambapo amesisitiza kuwa, "kama ambavyo mgogoro baina ya Wakurdi na Waturuki hauna umuhimu wowote kwao na mafuta ndicho kitu muhimu zaidi kwao, vivyo hivyo taifa la Iran halina umuhimu wowote kwa serikali ya Marekani."

Dakta Larijani ameeleza bayana kuwa, sera za Marekani zimejengeka katika udhalilishaji na kuwalazimisha wengine wasalimu amri na ndiposa inataka kudhibiti mafuta na gesi katika eneo.

Marekani imebakisha mamia ya askari wake Syria ili wadhibiti mafuta ya nchi hiyo ya Kiarabu

Amesisitiza kuwa, taifa lenye ustaarabu na historia ndefu la Iran katu halitakubali masharti na mashinikizo hayo ya Marekani.

Ameongeza kuwa, mataifa ya eneo hili yatatoa pigo kwa njama za utawala wa Trump za kuchochea migogoro Asia Magharibi kwa shabaha ya kudhibiti mafuta na gesi katika eneo.

Tags