Maana ya "kufutwa Israel" katika mtazamo wa Kiongozi Muadhamu
(last modified Fri, 15 Nov 2019 13:11:32 GMT )
Nov 15, 2019 13:11 UTC
  • Maana ya

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa sababu ya masaibu ya sasa ya Ulimwengu wa Kiislamu hususan hali ya kusikitisha ya Palestina ni udhaifu wa Umoja wa Waislamu.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika Baraza la Maulidi ya Mtume (saw) lililohudhuriwa na maafisa wa serikali, mabalozi wa nchi za kigeni na wageni waalikwa wanaoshiriki katika Mkutano wa 33 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran. Amesema kuwa msiba mkubwa zaidi wa Ulimwengu wa Kiislamu katika kipindi cha sasa ni kadhia ya Palestina na taifa lililofukuzwa kutoka kwenye nchi na makazi yake. 

Akitilia mkazo udharura wa kuwepo Umoja bina ya Waislamu, Ayatullah Khamene amesema: Hatua ya kwanza kabisa katika uwanja huu ni kujiepusha na mivutano baina ya jamii, tawala, madhehebu na kaumu za Waislamu na kuacha kushambuliana, na kuwa na umoja mkabala wa adui wao wa pamoja. 

Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (saw), Tehran

Hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuitangaza wiki moja ya baina ya tarehe 12 hadi 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal kuwa ni Wiki ya Umoja wa Kiislamu haikuwa harakati ya kisiasa, bali ni itikadi na imani madhubuti juu ya suala la kuwepo umoja na mshikamano wa Kiislamu kwa ajili ya kutatua matatizo yao, na suala hilo limeendelea kupewa umuhimu mkubwa na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita. Msimamo huo wa Iran una msingi katika mafundisho ya Uislamu yanayopinga dhulma, ubeberu na uonevu, na sababu kuu ya uadui na uhasama wa mabeberu dhidi ya Iran si kwa ajili ya nchi moja tu bali maadui hao wana uhasama na chuki dhidi ya Uislamu na nchi zote za Kiislamu. 

Misimamo na siasa madhubuti za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kulitetea taifa linalodhulumiwa la Palestina zinatokana na mafundisho halisi ya Uislamu yanayosisitiza wajibu wa kuwatetea watu wanaodhulumiwa, na hii leo hakuna watu wanaodhulumiwa na kukandamizwa zaidi kuliko taifa hilo. Kwa kufuata mafundisho hayo ya dini tukufu ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu hapo mwanzoni ilichukua hatua kadhaa za kuwatetea watu wa Palestina ikiwa ni pamoja na kufunga vituo na taasisi zote za Wazayuni mjini Tehran, kuanzisha ubalozi wa Palestina hapa nchini, kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi wa Ramadhani kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Quds, kuwasaidia Wapalestina kimaada, kiroho na kisiasa katika jumuiya za kikanda na kimataifa, na sisitizo la viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu la kufutwa utawala haramu wa Israel.

Taifa la Palestina linaendelea kudhulumiwa na kukandamizwa kwa kipindi cha miaka 70 sasa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa, njia ya kukomesha dhulma hiyo ni kuwapa wakazi asilia wa Palestina haki ya kujiamulia mambo yao wenyewe, suala ambalo linaoana na demokrasia. Wakati huo huo maadui wa Uislamu wamekuwa wakifanya mikakati ya kupotosha maana iliyokusudiwa na viongozi wa Iran wanaosisitiza "kufutwa utawala wa Kizayuni wa Israel". Maadui hao wanadai kuwa maana ya kufutwa Israel ni kuangamiza Mayahudi na kwa njia hiyo wanawataka walimwengu waamini kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uadui na kaumu ya Wayahudi. Katika hotuba yake ya leo kwenye hadhara ya mabalozi wa nchi za kigeni na wageni waalikwa katika mkutano wa Umoja wa Kiislamu Ayatullah Khamenei amekosoa njama hizo akisema: "Iran haina tatizo lolote na Mayahudi, na watu wakamu hiyo wanaishi kwa amani na utulivu hapa nchini kwetu." Amesema: Maana ya kufutwa Israel ni kuangamizwa utawala wa kutwishwa na wa Kizayuni; na wananchi wa Palestina, Waislamu, Wakristo na Wayahudi wakazi asili wa eneo hilo waweze kuchagua serikali yao wenyewe; na maajinabi, wahuni na wavamizi kama Netanyahu wafukuziwe mbali ili Wapalestina waongoze nchi yao; na jambo hili hatimaye litatimia."

Baadhi ya washiriki katika mkutano wa Umoja wa Kiislamu

Umoja na mshikamano halisi baina ya Waislamu ndiyo nguzo kuu ya kukomeshwa dhulma za maadui dhidi ya mataifa ya Kiislamu, na umoja huo hauwezi kupatikana kwa maneno matupu na misimo isiyotekelezwa ya baadhi ya nchi za Waislamu. Hivyo kuna udharura wa kuimarishwa umoja wa kivitendo baina ya mataifa, madhehebu na nchi za  Kiislamu na kujiepusha na mizozano na mivutano isiyo na maana.