Larijani: Marekani imekusudia kutoa pigo kwa wananchi wa Iran
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) ameashiria matasmhi ya uingiliaji ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ya kuunga mkono fujo na uharibifu wa kuchomwa mali za umma nchini Iran na kueleza kuwa: Viongozi wa Marekani wameazimia kutoa pigo kwa wananchi wa Iran.
Mike Pompeo ambaye nchi yake ina faili zito la kuingilia masuala ya ndani ya Iran ameashiria ghasia zilizotapakaa katika baadhi ya miji ya Iran na kudai kuwa Washington inawaunga mkono wananchi wa Iran katika suala hilo. Akizungumza leo Jumatatu katika kikao cha wazi cha Majlisi, Ali Larijani Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) ameongeza kusema kuwa: Bila ya aibu na huku akistafidi na fursa iliyojitokeza, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ameunga mkono wazi wazi kuchomwa moto mali za wananchi na kuitaja hatua yake hiyo kuwa ni kuwatetea wananchi wa Iran.
Larijani amesema kuwa lengo la Wamarekani si jingine isipokuwa kuibua ghasia na kuwaangamiza wananchi wa Iran na kusisitiza kuwa, wananchi wa Iran hata hivyo watazima njama hizo za maadui kwa kuwa kwao macho.
Baadhi ya maandamano ya amani ya wananchi wa Iran yamegeuka na kuwa fujo na ghasia baada ya kuingiliwa na baadhi ya wahuni kufuatia kupanda bei ya petroli hapa nchini. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei alisema jana katika darsa ya juu kabisa ya Fiqh kuhusu masuala yaliyojitokeza baada ya kutekelezwa mpango wa kubana matumiazi ya mafuta na kueleza kuwa: Ni wazi kuwa baadhi ya wananchi wametiwa wasiwasi na uamuzi huu lakini kufanya uharibifu na uchomaji wa mali za umma havifanywi na wananchi bali na wahuni. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa wale wote wanaopinga Mapinduzi na kuifanyia uadui Iran siku zote wanaunga mkono uharibu na machafuko kama hayo; na sasa pia wamejikita katika hujuma hizo.