Jeshi la Anga la Iran lafanya mazoezi makubwa ya kivita
Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linafanya mazoezi makubwa kwa lengo la kujiweka tayari kivita.
Mazoezi hayo ya kijeshi ambayo yemepewa jina la 'Walinzi wa Anga ya Velayat-98' yanafanyika katika eneo lenye ukubwa wa kilomita mraba 416,000 katika mkoa wa Semnnan kaskazini mwa Iran.
Katika mazoezo hayo kunafanyiwa majaribio mifumo ya kisasa ya makombora na rada ili kubaini uwezo wa zana hizo ambazo zimeundwa nchini Iran.
Akizungumza katika mazoezi hayo ya kijeshi siku ya Alhamisi, Kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga katika Jeshi la Iran Brigedia Jenerali Alireza Sabahi-Fard amewaonya maadui wasithubutu kukiuka anga ya Iran.
Itakumbukuwa kuwa, mwezi Juni mwaka huu, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilitungua ndege isiyo na rubani ya RQ-4 Global Hawk ambayo ni miongoni mwa ndege za kisasa kabisa za ujasusi za Marekani na inayogharimu dola milioni 220, baada ya kukiuka sheria na kuingia katika anga ya Iran.
Iran hufanya mazoezi makubwa ya kijeshi mara kwa mara ili kubaini uwezo na utayarifu wa vikosi vya ulinzi wa kujihami, na kwamba uwezo wake wa kijeshi si tishio kwa nchi yoyote bali sera zake za ulinzi zimejengeka katika msingi wa kujihami na kukabiliana na adui.