Iran na Qatar kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga tofauti
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema uhusiano wa kisiasa baina ya Iran na Qatar ni mzuri lakini nchi mbili hizo zina fursa ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa Doha na Tehran na katika nyuga mbalimbali zikiwemo za uchumi, biashara, utalii na sayansi.
Rais Rouhani alisema hayo jana Jumapili hapa Tehran katika kikao na waandishi wa habari akiwa pamoja na Amir wa Qatar, Tamim bin Hammad Aal Thani na kusisitiza kuwa, "Nchi fulani zimeiwekea Qatar vikwazo na kuiweka chini ya mzingiro, lakini Iran ilisimama na itaendelea kusimama na nchi hiyo ikiwa ni katika kutekeleza jukumu lake la ujirani mwema."
Dakta Rouhani amesisitiza kuwa, Iran na Qatar zina uhusiano mpana na wenye historia ndefu na kwa msingi huo, Tehran itaendelea kusimama bega ka bega na Doha katika hali zote.
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kuhusu kuundwa kamisheni ya pamoja ya ushirikiano baina ya Iran na Qatar ndani ya miezi michache ijayo na kubainisha kuwa, "Doha na Tehran zitasaini makubaliano kadhaa chini ya kamisheni hiyo, katika nyuga za biashara, uwekezaji na teknolojia."
Kwa upande wake, Tamim bin Hammad Aal Thani, Amir wa Qatar mbali na kupongeza uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi mbili hizi, amesisitiza haja ya kutumika mazungumzo na diplomasia katika kuipatia ufumbuzi migogoro inayozikabili nchi za Asia Magharibi.
Amiri wa Qatar aliwasili Tehran jana alasiri na kulakiwa na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Kasri la Sa'ad Abad hapa jijini Tehran.