Zarif: Uingereza inashirikana kibubusa na Marekani katika harakati zake za kigaidi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Uingereza inaifuata kipofupofu Marekani na kushiriki kibubusa katika harakati za kigaidi za Washington katika eneo la magharibi mwa Asia.
Mapema leo katika ukurasa wake wa Twitter Muhammad Javad Zarif ameashiria jinsi Uingereza ilivyofedheheshwa na Marekani katika vita vya Iraq na kuwaambia viongozi wa London kwamba: "Mnapaswa kuchagua njia ya izza na heshima kwa ajili ya kufanya mabadiliko na mlipe deni lenu kwa Wairani kwa mujibu wa amri iliyotolewa na mahakama."
Iran inaidai Uingereza pauni milioni 450 zinazohusiana na mikataba ya mauzo ya vifaru 1500 aina ya Chieftain na magari 250 ya deraya ambayo ilitiwa saini katika miaka ya 1974 na 1976.
Mwaka 2001 Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu iliitaka Uingereza kulipa deni hilo na hasara zilizosababishwa na mikataba hiyo lakini hadi sasa serikali ya London haijatekeleza uamuzi huo.