Zarif: Iran inaunga mkono haki za wananchi wa Palestina
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inaunga mkono haki za wananchi wa Palestina katika kuainisha hatima na mustakabali wao.
Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kusisitiza kwamba, Iran ipo pamoja na taifa la Palestina na inaunga mkono haki za taifa hili likiwemo suala la kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Baitul-Muqaddas.
Katika mazungumzo yake hayo na Mahmoud Abbas, Dakta Zarif amelaani pia mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne na kusema kuwa, Iran inafanya juhudi katika siasa zake kuhakikisha kuwa, katika mustakabali inazuia kufikiwa mipango na njama kama hizi dhidi ya wananchi wa Palestina.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inaunga mkono juhudi zinazofanyika za kupatikana maridhiano ya kitaifa baina ya Wapalestina.

Wiki iliyopita, Rais wa Marekani, Donald Trump alizindua mpango wa Muuamala wa Karne akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu.
Kwa mujibu wa mpango huo, Quds Tukufu itakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni; wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki tena ya kurejea katika ardhi za mababu zao na Palestina itamiliki tu ardhi zitakazosalia huko katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.