Iran yazima hujuma kubwa ya kiintaneti iliyolenga miundo msingi nchini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i59041-iran_yazima_hujuma_kubwa_ya_kiintaneti_iliyolenga_miundo_msingi_nchini
Naibu Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Iran ametangaza kuzumwa hujuma kubwa ya kiintaneti (cyber attack) dhidi ya miundo msingi nchini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 09, 2020 08:28 UTC
  • Iran yazima hujuma kubwa ya kiintaneti iliyolenga miundo msingi nchini

Naibu Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Iran ametangaza kuzumwa hujuma kubwa ya kiintaneti (cyber attack) dhidi ya miundo msingi nchini.

Akizungumza na waandishi habari,  Hamid Fattahi, Naibu Waziri wa TEHAMA Iran amesema: "Wadukuzi (Hackers) waliokodiwa, Jumamosi walitekeleza hujuma kubwa zaidi ya kiintaneti ambayo haijawahi kuhushudiwa katika historia ya Iran ambapo walilenga miundo msingi ya nchi."

Fattahi ameendelea kusema kuwa, wadukuzi hao walikuwa wanalenga kuvuruga kabisa mtandao wa mawasiliano ya intaneti lakini hujuma hiyo imezimwa kwa mafanikio makubwa. 

Aidha amesema wadukuzi hao wametumia mfumo wa hujuma aina ya DDoS na kwamba kompyuta zilizotumika kutekeleza hujuma hiyo zimebainika kuwa katika eneo la Asia Mashariki na Amerika Kaskazini. Mwezi Novemba mwaka 2019, Fattahi pia alitangaza kuwa, Iran ilifanikiwa kuzima wimbi la mashambulizi kupitia intaneti (cyber-attack) ambayo yalikuwa yametekelezwa na utawala haramu wa Israel kwa lengo la kuvuruga mitandao ya mawasiliano nchini.

Mwezi Juni mwaka 2019, Waziri wa Habari na Teknolojia ya Mawasiliano wa Iran, Mohammad Javad Azari Jahromi alisema mashambulizi ya kompyuta ya Marekani dhidi ya mfumo wa makombora wa Iran yalishindwa kuleta utata wowote na kwamba mwaka jana pekee Tehran ilifanikiwa kuzima makumi ya mamilioni ya mashambulizi ya kompyuta dhidi yake.

Waziri Jahromi alisema kuwa kwa muda mrefu sana Iran imekuwa ikikabiliana na ugaidi wa mashambulizi ya kompyuta kutoka kwa adui na mwaka 2018 ilifelisha mashambulizi milioni 33 kwa kutumia mfumo wake maalumu wa kitaifa wa kujilinda na mashambulizi ya kompyuta.