Utawala wa Israel wamfunga jela kiongozi wa Harakati ya Kiislamu
Mahakama ya utawala haramu wa Israel imemfunga jela kiongozi wa Harakati ya Kiislamu, Sheikh Raed Salah, kwa miezi 28 kwa tuhuma za 'kuchochea ugaidi'.
Katika hukumu iliyotolewa Jumatatu, mahakama imedai kuwa alitoa hotuba za kichochezi mnamo Julai 2017 baada ya Mpalestina mmoja kuwaua wanajeshi wawili wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika uwanja wa Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem).
Salah amepinga tuhuma dhidi yake na kusema hazina msingi wowote na kuwa kesi dhidi yake haikuzingatia ukweli.
Sheikh Salah amekuwa akisumbuliwa na wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na misimamo yake imara ya kutetea ukombozi wa Palestina. Alikamatwa Agosti 2017 nyumbani kwake katika mji wa Umm al Fahm na kufunguliwa mashtaka ya uchochezi tuhuma ambazo amezikanusha. Mwaka 2015, Israel ilimpiga marufuku Salah kusafiri nje ya nchi kwa sababu zilizotajwa kuwa ni za 'usalama wa taifa.'
Sheikh Salah alianzisha Harakati ya Kiislamu ya Palestina ndani ya utawala haramu wa Israel mwaka 1971 na inakadriwa kuwa na wanachama 20,000. Harakati hiyo ilipigwa marufuku na Israel mwaka 2015. Harakati hiyo ilipata umaarufu kutokana na kazi zake za kutoa misaada na huduma zingine za kijamii mionongoni mwa Waarabu ambao ni raia wa utawala haramu wa Israel.