Tume ya Uchaguzi Iran: Kampeni za uchaguzi wa Bunge zimeanza leo Alkhamisi
Tume ya Uchaguzi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran imetangaza kuwa, kampeni za uchaguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, yaani Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu zimeanza leo Alkhamisi.
Taarifa ya Tume ya Uchaguzi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran imeeleza kuwa, wagombea wote ambao wamepasishwa kwa ajili ya uchaguzi ujao wa Bunge wana fursa kuanzia leo Alkhamisi ya kufanya mikutano na kampeni zao za kujinadi kwa wapiga kura..
Taarifa zaidi zinasema kuwa, kampeni hizo za uchaguzi wa Bunge zitamalizika Alkhamisi ijayo ya tarehe 20 Februari yaani siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi huo siku ya Ijumaa ya tareher 21 Februari.
Wapiga kura watajitokeza siku hiyo katika majimbo 208 ya uchaguzi kote nchini Iran kwa ajili ya kuwachagua wabunge 290 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu. Siku hiyo kutafanyika pia uchaguzi mdogo wa Baraza la Tano la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi katika majimbo matano ya Tehran, Fars, Khorasan ya Kaskazini, Khorasan ya Razavi na Qum. Kufanyika uchaguzi ni moja ya misingi ya ushirikishaji umma kisiasa na kuwa na utawala unaotokana na ridhaa ya wananchi.
Kwa mujibu wa Ibara ya 62 ya Katiba, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu inaundwa kutokana na wawakilishi wa wananchi, ambao huchaguliwa moja kwa moja kwa kura za siri kwa ajili ya kipindi cha miaka minne.