Mousavi: Iran itatoa jibu kali kwa hatua yoyote ya kijinga ya Israel
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Iwapo utawala wa Kizayuni wa Israel utatekeleza uvamizi au hatua yoyote ya kijinga dhidi ya maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Syria na katika eneo, basi utawala huo utapokea jibu kali ambalo litakuwa la majuto."
Siku ya Jumatano, Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alitoa tamko hilo kufuatia madai na vitisho vya afisa mmoja wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa: "Msingi na utambulisho wa utawala huo katika kipindi cha miaka 70 ya kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina na nchi jirani umekuwa ni mauaji, uporaji mali, ugaidi na uvamizi."
Mousavi ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko nchini Syria kufuatia mwaliko rasmi na mapatano na serikali ya nchi hiyo kwa lengo la kukabiliana na magaidi wanaopata himaya ya Marekani na Israel. Ameongeza kuwa, Iran katu haitasita au kulegea hata lahadha moja katika kulinda uwepo wake Syria na katika kutetea usalama wake wa kitaifa na maslahi yake katika eneo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa Iran itafuatilia vitisho na matamshi ya kutaka vita ya utawala ghasibu wa Israel katika taasisi za kimataifa.
Naftali Bennett, Waziri wa Vita wa Utawala wa Kizayuni amekariri madai yasiyo na msingi yaliyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kusema Israel daima inatekeleza jitihada za kuidhoofisha Iran ili kuilazimisha iondoke Syria.