Shamkhani: Waislamu watafanya sherehe mjini Damacus Syria, za kutimuliwa Wazayuni Palestina
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran iko nchini Syria kwa ombi rasmi la serikali ya nchi hiyo na kwamba Waislamu watafanya sherehe mjini Damascus kusherehekea kutimuliwa Wazayuni katika eneo hili.
Jana Alkhamisi, Ali Shamkhani aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko nchini Syria kwa mwaliko wa serikali halali ya nchi hiyo na kwamba Waislamu wa eneo hili watasherehekea mjini Damascus kutimuliwa Wazayuni katika ardhi za Palestina hata kabla ya kumalizika majukumu ya Iran huko Syria.
Mgogoro wa Syria ulianzishwa mwaka 2011 kwa kumiminwa magenge mengi mno ya kigaidi ndani ya ardhi ya nchi hiyo kutoka pembe mbalimbali za dunia kwa uungaji mkono wa madola ya kibeberu ya Magharibi, majirani wa Syria kama vile Uturuki na nchi za Kiarabu ili kujaribu kulivunja nguvu taifa la Syria ambalo liko mstari wa mbele katika kupambana na Wazayuni wanaokikalia kwa mabavu Kibla cha Kwanza cha Waislamu, Masjidul Aqswa na maeneo mengine ya Palestina.
Hata hivyo kwa kuungwa mkono na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia, Syria imefanikiwa kukomboa sehemu kubwa mno ya ardhi ya nchi hiyo na kuwatimua magaidi waliokuwa wakifanya jinai zisizo na kifani na za kila namna dhidi ya wananchi na maafisa wa serikali ya Syria.
Sehemu zilizosalia hivi sasa bila ya kufurushwa magaidi huko Syria, ni baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo hasa baadhi ya maeneo ya mkoa wa Idlib ambapo taarifa zinasema kuwa, zaidi ya nusu ya mkoa huo umeshakombolewa na sasa hivi wanajeshi wa Syria na waitifaki wao wanaendeleza mapambano ya kuyafurusha kikamilifu magenge ya kigaidi katika kila shibri ya ardhi ya Syria.