Iran yatengeneza kifaa cha kupima kirusi cha Corona
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i59349-iran_yatengeneza_kifaa_cha_kupima_kirusi_cha_corona
Wataalamu Wairani wamefanikiwa kutengeneza kifaa maalumu cha kupima kirusi cha Corona. Kifaa hicho ni cha kwanza cha aina hiyo kuundwa nchini Iran.
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Feb 24, 2020 01:13 UTC
  • Iran yatengeneza kifaa cha kupima kirusi cha Corona

Wataalamu Wairani wamefanikiwa kutengeneza kifaa maalumu cha kupima kirusi cha Corona. Kifaa hicho ni cha kwanza cha aina hiyo kuundwa nchini Iran.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, kifaa hicho cha kupima kirusi cha Corona kimeundwa na wataalamu Wairani katika Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kifaa hicho kilichoundwa nchini Iran kina uwezo wa kubaini iwapo mwanadamu ana kirusi cha  Corona mwilini na hivyo kutoa mchango mkubwa katika kukabiliana na kirusi cha Corona ambacho pia kinajulikana kama COVID-19.

Tangu kuthibitishwa kwa visa vya kwanza Desemba 2019, homa ya COVID -19 ya kirusi cha Corona ilisambaa na kuwa dharura kuu ya kiafya duniani, na kuua mamia ya watu na kuambukiza maelefu ya wengine.

Wafanyakazi wa Afya China wakipima kiwango cha joto cha mpita njia ikiwa ni katika jitihada za kukabiliana na kirusi cha Corona

Homa hiyo iliripotiwa mara ya kwanza katika mji wa Wuhan mkoani Huabei mashariki mwa China na sasa mbali na kuenea katika mikoa 30 nchini China homa hiyo ya Corona imeenea katika zaidi ya nchi 30 zikiwemo Iran, Marekani, Uingereza, Australia, Italia, Thailand, Korea Kusini, Japan, Canada, Ufaransa, Umoja wa Falme za Kiarabu au Imarati.

Kwa mujibu wa takwimu, hadi sasa watu wasiopungua 79,000 wameambukizwa kirusi cha Corona duniani, aghalabu wakiwa nchini China na miongoni mwao 18,000 wamepata nafuu na kuruhusiwa kuondoka hospitalini huku wengine 2, 400 wakipoteza maisha.