Watu waliopoteza maisha kwa Corona nchini Iran wafikia 12
Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Matibabu ya Iran imetangaza habari ya kuongezeka idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na virusi vya Corona humu nchini.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Dk Kianoosh Jahanpour, Mkuu wa Kituo cha Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari cha Wizara ya Afya ya Iran ametangaza leo kuwa, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya Corona hadi leo Jumatatu humu nchini ni watu 61 huku 12 kati yao wakiwa wameshafariki dunia. Hadi jana Jumapili, idadi ya watu waliokuwa wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo nchini Iran walikuwa ni 43 ambapo wanane kati yao walikuwa wameshafariki dunia.
Jana Rais Hassan Rouhani alitoa amri kwa waziri wa afya afanye juhudi zote na kutumia suhula zote zilizopo nchini kuhakikisha kuwa ugonjwa huo unadhibitiwa haraka. Leo Jumatatu, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, Meja Jenerali Hossein Salami amezungumza kwa njia ya simu na waziri wa afya na kumueleza kuwa jeshi hilo liko tayari kutumia suhula zake zote kufanikisha mapambano dhidi ya virusi vya Corona humu nchini.
Huku hayo yakiripotiwa, wataalamu wa Iran wamefanikiwa kutengeneza kifaa maalumu cha kupima kirusi cha Corona. Kifaa hicho ni cha kwanza cha aina hiyo kuundwa humu nchini. Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, kifaa hicho cha kupima kirusi cha Corona kimeundwa na wataalamu Wa Iran katika Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Tangu kuthibitishwa kesi ya kwanza mwezi Disemba 2019, homa ya COVID -19 ya kirusi cha Corona imesambaa katika kona mbalimbali za dunia na kuwa dharura kuu ya kiafya ulimwenguni. Hadi sasa imeshauua mamia ya watu na kuambukiza maelfu ya wengine.