Zarif: Marekani inawashikilia mateka wanasayansi wa Kiirani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameituhumu serikali ya Marekani kwamba haiwapi wasomi na wanasayansi wa Iran wanaoshikiliwa katika jela za nchi hiyo ruhusa ya kupata matibabu licha ya wimbi kubwa la maambukizi ya sasa ya virusi vya corona.
Ijumaa ya jana Muhammad Javad Zarif amesambaza picha ya ripoti ya gazeti la The Guardian la Uingereza kuhusu hali ya wanasayansi na wasomi wa Iran wanaoshikiliwa mahabusu huko Marekani na kuandika kuwa: Marekani inawashikilia mateka wasoma kadhaa wa Iran bila ya tuhuma yoyote au kwa tuhuma zisizo na msingi eti za kukiuka vikwazo, na imekataa kuwaachia huru hata baada ya mahakama zake kutupilia mbali tuhuma hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Marekani imewanyika hata ruhusa ya kupata matibabu wasomi hao wa Kiirani wasio na hatia yoyote wanaoshikiliwa katika jela za kutisha katika kipindi hiki cha maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
Akiambatanisha na ripoti ya gazeti la The Guardian la Uingereza kuhusu hali mbaya ya mwanasayansi wa Iran, Sirous Asghari anayeshikiliwa jela huko Marekani, Dakta Zarif ameandika kwenye mtandao wa Twitter akisema: Mwachieni huru raia wetu.
Sirous Asghari, msomi wa Kiirani anayeshikiliwa katika mahabusu ya Idara ya Uhamiaji ya Marekani (ICE) ameliambia gazeti la Guardian la Uingereza kwamba, maafisa wa jela hilo wanawanyima kwa makusudi wafungwa barakoa (mask) na vitakasa (sanitizer) ili waangamie wenyewe kwa maradhi ya COVID-19.
Ijumaa ya jana gazeti la Guardian liliandika kuwa, Dokta Sirous Asghari anaendelea kushikiliwa katika jela la Idara ya Uhamiaji ya Marekani licha ya mahakama ya nchi hiyo kuthibitisha kwamba, hana hatia yoyote.
Mwanasayansi huyo wa Iran ameliambia gazeti la The Guardian kwamba yumkini akafariki dunia yeye na mahabusu wenzake kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.