Salehi: Wakala wa IAEA usiwe wenzo wa mashirika ya kijasusi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60183-salehi_wakala_wa_iaea_usiwe_wenzo_wa_mashirika_ya_kijasusi
Mkuu wa Shirka la Atomiki la Iran amesema kuhusu madai yaliyotolewa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ambayo sasa yanafuatiliwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kwamba wakala huo haupasi kuwa wenzo unaokamilisha kazi za mashirika ya ujasusi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 05, 2020 06:18 UTC
  • Ali Akbar Salehi
    Ali Akbar Salehi

Mkuu wa Shirka la Atomiki la Iran amesema kuhusu madai yaliyotolewa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ambayo sasa yanafuatiliwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kwamba wakala huo haupasi kuwa wenzo unaokamilisha kazi za mashirika ya ujasusi.

Ali Akbar Salehi ameongeza kuwa, kwa hatua hiyo, wakala wa IAEA umetia mashakani na kuzusha maswali mengi kuhusiana na nafasi yake ya usimamizi huru wa shughuli za nyuklia na inaonesha kuwa haufanyi kazi kwa misingi ya sheria na kanuni.

Salehi amesema kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki haupasi kuunga mkono harakati za kijasusi zinazokiuka haki na mamlaka ya kujitawala ya nchi mbalimbali na sheria zinazotawala mahusiano ya kimataifa. 

Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amesema kuwa, shughuli za kuzalisha nishati ya nyuklia hapa nchini zinafanyika bila ya kizuizi chochote na kwamba kwa mwenendo huu wa kupunguza uwajibikaji wa Iran kwa mujibu wa makubaliano ya kundi la 5+1, kuna uwezekano wa kutazamwa upya masuala mengine ya kisheria kama utekelezaji wa protokali ziada na hata mkataba wa NPT. 

Ali Akbar Salehi

Tarehe 5 Januari mwaka 2019 Iran ilianza kupunguza utekelezaji wake wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baada ya nchi za Magharibi wanachama katika mkataba huo kukengeuka vipengele vyake. 

Vifungu nambari 26 na 36 vya mkataba huo vinasisitiza kuwa, iwapo upande mmoja wa JCPOA hautaheshimu makubaliano hayo, Iran pia itakuwa na haki ya kuacha kuyatekeleza.