Watoto wachanga 14 wafariki katika ajali ya moto iliyotokea hospitalini Pakistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140978-watoto_wachanga_14_wafariki_katika_ajali_ya_moto_iliyotokea_hospitalini_pakistan
Watoto wachanga wasiopungua14 wamefariki dunia katika moto uliozuka kwenye chumba cha watoto cha hospitali ya serikali katika mji mkuu wa Pakistan, Islamabad, huku Waziri Mkuu Shehbaz Sharif akitangaza kuwa ameshaamuru uchunguzi ufanyike kuhusu ajali hiyo.
(last modified 2026-08-26T11:16:29+00:00 )
Aug 26, 2026 11:15 UTC
  • Watoto wachanga 14 wafariki katika ajali ya moto iliyotokea hospitalini Pakistan

Watoto wachanga wasiopungua14 wamefariki dunia katika moto uliozuka kwenye chumba cha watoto cha hospitali ya serikali katika mji mkuu wa Pakistan, Islamabad, huku Waziri Mkuu Shehbaz Sharif akitangaza kuwa ameshaamuru uchunguzi ufanyike kuhusu ajali hiyo.

Moto huo umetokea leo Jumatano katika ghorofa ya tatu ya Kituo cha Mama na Mwana cha hospitali ya Taasisi ya Sayansi ya Tiba ya Pakistan (PIMS).

Mtangazaji wa Geo TV wa eneo hilo, amevinukuu vyanzo vya hospitali na kutangaza kuwa idadi halisi ya vifo ni 15.

Kwa mujibu wa televisheni hiyo, moto huo, ambao ulianza dakika chache kabla ya saa moja asubuhi kwa saa za huko, ulifanikiwa kuzimwa. Taarifa ya chombo hicho cha habari imeongeza kuwa, ni mtoto mmoja tu ndiye aliyewahi kuokolewa.

Katika taarifa yake kupitia mtandao wa kijamii wa X, Waziri Mkuu wa Pakistan ametoa "rambirambi zake za dhati kwa familia zilizofiwa" na kuagiza mamlaka husika kufanya "uchunguzi wa haraka".

Sharif ameahidi kwamba wale waliohusika watakabiliwa na "hatua kali kabisa".

Geo TV imenukuu vyanzo vya uokoaji vikisema, moto huo huenda ulisababishwa na hitilafu za umeme katika kitengo cha kiyoyozi kilichokuwa hakifanyi kazi vizuri.

Moto kwenye majengo ni miongoni mwa ajali za kawaida kutokea nchini Pakistan, ambapo kanuni za usalama na kanuni za ujenzi huwa mara nyingi zinapuuzwa au hazitekelezwi ipasavyo.

Mnamo mwezi Januari mwaka huu, watu wasiopungua 65 walifariki wakati moto mkubwa ulipolikumba eneo la maduka lililofurika watu katika mji wa bandari wa kusini wa Karachi.

Moto wa leo ni moja ya moto uliotokea hospitalini ambao umesababisha maafa makubwa zaidi ya roho za watu katika historia ya Pakistan.

Wakati serikali ya Islamabad inatoa ruzuku ya matibabu kupitia hospitali za umma, sekta yenyewe ya serikali ingali ina ufadhili mdogo, uendeshaji usiorodhisha na inaelemewa na idadi kubwa ya watu kupita kiasi…/