Zarif: Marekani imepoteza fursa ya kuuacha uraibu wake wa vikwazo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, virusi vya corona ilikuwa fursa nzuri kwa Marekani ya kuacha uraibu ilionao wa kuweka vikwazo, lakini Washington imepoteza fursa hiyo.
Mohammad Javad Zarif amesema katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter kwamba, licha ya vikwazo vya kidhalimu vya Marekani, lakini kwa kutegemea rasilimaliwatu, uwezo wake wa kisayansi na marafiki wa nje, Iran imeweza kupiga hatua kubwa katika kukabiliana na virusi vya corona.
Katika ujumbe wake huo, Zarif ameongeza kuwa, ugonjwa wa COVID-19 ulikuwa fursa kwa Marekani ya kuacha uraibu wake wa kuweka vikwazo, lakini kutokana na kutofanya hivyo, Marekani itabaki ikikumbukwa kwa ubaya katika fikra za wananchi wa Iran.

Katika wiki za karibuni na kufuatia kuzuka kwa janga la COVID-19 duniani kote, shakhsia mbali mbali wa kimataifa pamoja na nchi kadhaa duniani zikiwemo Uturuki, Russia, Pakistan na China wamekuwa wakitoa miito ya kuitaka Marekani iondoe vikwazo vyake haramu, vya upande mmoja na vya kidhalimu ilivyoiwekea Iran, lakini viongozi wa Washington wangali wameng'ang'ania msimamo wao wa kuendeleza vikwazo hivyo kupitia sera ya utoaji mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu sambamba na kutangaza vikwazo vingine vipya kila uchao.
Vikwazo hivyo vinavyojumuisha bidhaa za msingi zikiwemo hata dawa na zana za tiba vimewasababishia matatizo mbalimbali wananchi wa Iran hususan wale wanaoatilika kwa ugonjwa wa COVID-19.../