Zarif: Dunia nzima hivi sasa inateseka kwa ubeberu wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60396-zarif_dunia_nzima_hivi_sasa_inateseka_kwa_ubeberu_wa_marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelezea kusikitishwa kwake na uamuzi wa Marekani wa kulikatia misaada Shirika la Afya Duniani (WHO) na kusema kuwa hivi sasa dunia inapita kwenye kipindi cha mateso ya ubeberu wa Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 15, 2020 20:14 UTC
  • Zarif: Dunia nzima hivi sasa inateseka kwa ubeberu wa Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelezea kusikitishwa kwake na uamuzi wa Marekani wa kulikatia misaada Shirika la Afya Duniani (WHO) na kusema kuwa hivi sasa dunia inapita kwenye kipindi cha mateso ya ubeberu wa Marekani.

Dk Mohammad Javad Zarif alisema hayo jana kwenye mtandao wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, sasa hivi dunia imo katika kujifunza kitu ambacho Iran inakijua na kupata uzoefu wake kwa muda wote huu wa umri wa Jamhuri ya Kiislamu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, vitisho, upayukali na majigambo ya utawala wa Marekani si uraibu tu, bali ni uovu ambao unaua watu. 

Donald Trump

 

Amma kuhusiana na uamuzi wa Marekani wa kulikatia misaada ya fedha Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Zarif amesema: Kama ilivyojiri kwa "mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa" yaliyowekwa na Marekani dhidi ya Iran, kulikatia misaada shirika la WHO tena wakati huu ambapo dunia nzima imehamanishwa na ugonjwa wa corona, hakutakuwa na matunda mengine isipokuwa kuzidi kuichafulia jina tu Marekani. 

Rais wa Marekani, Donald Trump ametekeleza kivitendo vitisho vyake dhidi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kulikatia misaada ya kifedha shirika hilo la Umoja wa Mataifa tena katika kipindi hiki ambacho dunia imekumbwa na changamoto kubwa sana za kimatibabu yaani vita dhidi ya ugonjwa wa corona ambao jina lake rasmi ni COVID-19.

Donald Trump analituhumu Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa linaipendelea China na anadai kuwa eti shirika hilo halikuitahadharisha Marekani kuhusu kirusi cha corona.