Iran inaongoza duniani katika kunasa dawa za kulevya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60666-iran_inaongoza_duniani_katika_kunasa_dawa_za_kulevya
Katibu wa Idara ya Kupambana na Dawa za Kulevya katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pamoja na kuwepo vikwazo, Iran inaongoza katika kunasa idadi kubwa zaidi ya dawa za kulevya duniani; ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita imeweza kunasa tani 950 za aina kadhaa za dawa za kulevya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 29, 2020 00:50 UTC
  • Iran inaongoza duniani katika kunasa dawa za kulevya

Katibu wa Idara ya Kupambana na Dawa za Kulevya katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pamoja na kuwepo vikwazo, Iran inaongoza katika kunasa idadi kubwa zaidi ya dawa za kulevya duniani; ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita imeweza kunasa tani 950 za aina kadhaa za dawa za kulevya.

Akizungumza Jumanne, Eskandar Muumini, Katibu Mkuu wa Idara ya Kupambana na Dawa za Kulevya ya Iran amesema Umoja wa Mataifa umeishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na jitihada zake za kupambana na dawa za kulevya. Ameongeza kuwa,  katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Polisi ya Iran imenasa tani 800 za dawa za kulevya au mihadarati huku Wizara ya Usalama wa Taifa ikinasa tani 100 nao maafisa wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi, Basiji, wakinasa tani 30.

Bw. Muumini ameongeza kuwa asilimia 74 ya mihadarati iliyonaswa ilitokana na taarifa za  siri na kwamba asilimia 76 ya mihadarati hiyo ilipatikana katika mikoa ya mashariki mwa nchi.

Eskandar Muumini

Katibu Mkuu wa Idara ya Kupambana na Dawa za Kulevya ya Iran amebaini kuwa kote duniani kuna watumizi milioni 300 wa mihadarati na kuongeza kuwa:  " Kila mwaka takribani watu 450,000 hupoteza maisha kutokana na matumizi ya mihadarati na miongoni mwao 70,000 ni Wamarekani na karibu 3,000 ni kutoka Iran.

Bw. Muumini ameendelea kusema kuwa, Ujumbe wa Kimatiafa wa Kudhibiti Mihadarati umeishukuru rasmi Iran kutokana na jitihada zake za kuwapa matibabu na makao waraibu wa mihadarati na kuongeza kuwa: "Pamoja na kuwepo vikwazo vilivyo kinyume cha sheria, Iran inatumia uwezo wake wote kuokoa maisha ya wanadamu."