Feb 09, 2024 08:14 UTC
  • Muendelezo wa juhudi za Iran katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya

Mkuu wa Polisi wa Iran, ameeleza kuridhishwa kwake na juhudi za kitengo cha kupambana na dawa za kulevya cha kikosi hicho, na kusema jeshi hilo liangamiza watu 230 waliokuwa wahusika wakuu katika biashara haramu ya dawa za kulevya na wakati huo huo kunasa tani 500 za afyuni katika kipindi cha miezi 10 iliyopita.

Kutokana na kupakana na chanzo kikuu cha uzalishaji wa dawa za kulevya duniani yaani Afghanistan, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekabiliwa na magendo ya dawa za kulevya kwa miaka mingi. Hii inatokana na wasafirishaji haramu wa dawa za kulevya kutaka kutumia ardhi ya Iran kwa ajili ya kusafirisha dawa za kulevya kuuelekea barani Ulaya na kwingineko duniani.

Brigedia  Jenerali Ahmadreza Radan

Ni dhahiri kwamba kuingia kwa sehemu ya dawa za kulevya katika jamii na kupanuka kwa wigo wa uraibu na madhara yanayotokea, haswa kwa vijana, ni tishio kubwa kwa afya ya jamii. Ijapokuwa Iran imechukua hatua kama vile kujenga ukuta kwenye mpaka wa kilomita 900 na Afghanistan, kuanzisha vituo vya mpaka, kufunga kamera, seng'ege, na kuchimba mahandaki kwenye mipaka yake ya mashariki ili kukabiliana na wafanyabiashara haramu na kuzuia usafirishaji wa mihadarati, lakini inataka ushiriki na usaidizi wa nchi zote na taasisi za kimataifa na kutoa mchango wa kifedha kwa lengo la kuondokana na tatizo la kimataifa la uzalishaji mihadarati, biashara na usafirishaji wa mihadarati na tatizo  la uraibu.

Brigedia Jenerali Ahmadreza Radan, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi la Iran, akizungumza karibuni pambizoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Polisi wa Kupambana na Dawa za Kulevya aliwaambia waandishi wa habari kwamba Iran imezidisha mapambano dhidi ya mihadarati. Alisema kwamba kwa juhudi za maafisa wa kitengo hiki, katika kipindi cha miezi 10 iliyopita, takriban tani 500 za dawa za kulevya zimenaswa, ambayo ni rekodi ya dunia. Aidha amesema watu 230 ambao walikuwa vinara wa ulanguzi wa dawa za kulevya wameuawa katika kipindi hicho.

Askari wa Marekani akilinda shamba la mihadarati Afghanistan 

Jenerali Radan amesema kuwa mpango ulio mbele ya kitengo cha kupambana na mihadarati cha Iran ni kuzidisha kukabiliana na walanguzi wa dawa za kulevya katika maeneo yanayopakana na Afghanistan na Pakistan nchi ambazo ni vituo vikuu vya uzalishaji na usafirishaji wa mihadarati,
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi kkaribuni ya makao makuu ya kitengo cha kupambana na mihadarati ya Iran, askari wa kikosi cha ulinzi wa mpakani mashariki mwa nchi walifanikiwa kugundua na kukamata kilo 1083 za dawa za kulevya katika operesheni iliyofanyika siku chache zilizopita.
 Justin Teddy mkuu wa idara ya huduma za sayansi na maabara katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Madawa ya Kulevya na Uhalifu mwezi uliopita, katika mkutano na Alireza Kazemi, Naibu Katibu Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Iran, aliishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na mipango yake ya kina katika mapambano dhidi ya mihadarati

Katika kikao hicho alitoa wito wa matumizi ya tajriba muhimu za Tehran katika uwanja huu. Katika mkutano huu, ilitangazwa kuwa karibu 30% ya ugunduzi wa heroini duniani unafanywa na Iran. Kulingana na taarifa za Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Uhalifu na Madawa ya Kulevya, ongezeko la biashara haramu ya dawa za kulevya husababisha vifo vya takriban watu 100,000 kila mwaka.

Shamba la mihadarati (mpopi) Afghanistan

Kwa kutilia maanani ujirani wa Iran na Afghanistan nchi ambayo ni kituo kikubwa zaidi cha uzalishaji wa dawa za kulevya, Jamhuri ya Kiislamu mbali na kutumia mabilioni ya fedha, imetoa muhanga takriban mashahidi 4,000 na maveterani zaidi ya 12,000 kwa ajili ya kulinda jamii ya wanadamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya makao makuu ya kitengo cha kupambana na mihadarati ya Iran, uwepo wa miaka 20 wa wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Afghanistan umekuwa moja ya mambo muhimu zaidi katika ongezeko la uzalishaji wa dawa za kulevya. Mwaka 2001 wakati Marekani ilipoanza kukalia kwa mabavu Afghanistan jumla ya uzalishaji wa madawa ya kulevya wa nchi hii ilikuwa takribani tani 200, lakini mwaka 2021,uzalishaji huu uliongezeka hadi tani 9,500, ambayo ina maana kwamba uzalishaji wa madawa ya kulevya uliongezeka mara hamsini wakati wa kuwepo kwa Wamarekani nchini Afghanistan.

Mtazamo wa mielekeo ya kisiasa ya Afghanistan katika miongo miwili iliyopita unaonyesha kuwa, sababu ya kuigeuza nchi hii kuwa moja ya nguzo kubwa za uzalishaji na biashara haramu ya dawa za kulevya ni siasa haribifu ambayo Marekani imekuwa ikifuatilia huko Magharibi mwa Asia.

Sasa ikiwa imepita takribani miaka miwili na nusu tangu kumalizika kwa uwepo wa jeshi la Marekani nchini Afghanistan, takwimu zinaonyesha kuwa kilimo cha mihadarati kipmepungua katika nchi hii.

Kupungua huku kwa kiasi fulani kunahusiana na juhudi za serikali ya Taliban na kwa kiasi fulani kunatokana na kushadidi mapambano ya Iran dhidi ya biashara ya dawa za kulevya katika maeneo ya mipakani.

Katika hali hiyo, msaada wa kifedha na wa taasisi za kimataifa kama vile Ofisi ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Madawa ya Kulevya na Uhalifu kwa wakulima wa Afghanistan kukuza mazao mengine badala ya mpopi  na usaidizi  kwa serikali iliyoko Kabul ni mambo yanayoweza kuwa suluhisho linalofaa kwa kupunguza uzalishaji wa dawa za kulevya katika nchi hii. Hakuna shaka kuwa  kupungua kwa uzalishaji dawa za kulevya Afghanistan ni kwa faida wa raia wa nchi hiyo na watu katika sehemu zote za dunia.

Tags