Israel yapata hasara ya dola bilioni 66 katika vita vya Ghaza na Lebanon
(last modified Tue, 08 Oct 2024 05:56:56 GMT )
Oct 08, 2024 05:56 UTC
  • Israel yapata hasara ya dola bilioni 66 katika vita vya Ghaza na Lebanon

Takwimu mpya za Benki Kuu ya utawala wa Kizayuni zinaonesha kuwa, Israel imeshapata hasara ya dola bilioni 66 za Kimarekani katika vita vyake dhidi ya Ghaza na Lebanon.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika kipindi hiki cha mwaka mmoja uliopita, Marekani imeshaupa utawala wa Kizayuni karibu dola bilioni 18 za kufanyia jinai dhidi ya Wapalestina na Walebanon.

Shirika la habari la FARS limenukuu ripoti ya gazeti la Foreign Policy la Marekani ambalo limeandika kuwa, hasara uliyopata utawala wa Kizayuni hadi hivi sasa kutokana na vita vya Ghaza na Lebanon haipungui dola bilioni 66 za Kimarekani.

Taarifa ya Benki Kuu ya utawala wa Kizayuni imeongeza kuwa, hasara iliyopata Israel katika vita vyake dhidi ya Ghaza na Lebanon ni sawa na uzalishaji wa asilimia 12 wa malighafi ndani ya utawala huo pandikizi.

Utawala wa Kizayuni unaendelea kupata hasara ya makumi ya mabilioni ya dola kutokana na vita vya Ghaza na Lebanon

 

Uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Brown cha nchini Marekani ambapo matokeo ya uchunguzi huo yalitangazwa jana Jumatatu unaonesha kuwa, tangu vilipoanza vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza, Marekani imeshaipa Israel msaada wa kijeshi usiopungua dola bilioni 17.9 ili kufanya jinai na ukatili dhidi ya wanawake, watoto na watu wasio na hatia huko Ghaza.

Baada ya kupita mwaka mmoja tangu Israel ianzishe mauaji ya kikatili kwenye Ukanda wa Ghaza wachambuzi wa mambo wanazidi kusisitiza kuwa, kama si uungaji mkono wa pande zote wa kisiasa na kijeshi wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, Wazayuni wasingeliweza kabisa kufanya jinai wanazofanya huko Ghaza na Lebanon.