Oct 08, 2024 03:40 UTC
  • Fatemeh Mohajerani
    Fatemeh Mohajerani

Msemaji wa serikali ya Iran, Fatemeh Mohajerani, amesema Iran kamwe haitarudi nyuma katika kutetea maslahi yake ya kitaifa huku akiuonya utawala wa Kizayuni wa Israel usithubutu kuvuka mipaka.

Akizungumza na IRNA siku ya Jumatatu, Mohajerani alipongeza shambulio la hivi karibuni la majeshi ya Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, lililopewa jina la Operesheni Ahadi ya Kweli II - ambalo amesema "limerejesha fahari ya kitaifa."

Ameongeza kuwa kama mkuu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian alitoa ridhaa yake kwa operesheni hiyo, akibainisha kuwa waziri wa ulinzi pia ana jukumu muhimu katika baraza hilo.

Oktoba Mosi, Iran ilivurumisha mamia ya makombora yaliyolenga ngome za kijeshi na kijasusi na vituo kadhaa vya usalama katika maeneo anayokaliwa kwa mabavu ya Palestina (Israel).

Makombora ya Iran yakishuka katika ngome za kijeshi na kijasusi za 'Israel'

Akiashiria mauaji ya Israel dhidi ya Ismail Haniyeh, aliyekuwa mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, (HAMAS) mjini Tehran, Mohajerani amesema hadi miezi miwili baada ya kuuawa shahidi Haniyeh, katika hujuma iliyoteklezwa na Israel, serikali ya Iran ilijizuia kwa sababu ya matarajio ya kusitishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Msemaji huyo wa serikali ya Iran amesisitiza zaidi kuwa, katika kipindi cha miaka minane ya Kujihami Kutakatifu, (vita vya Saddam dhidi ya Iran) Jamhuri ya Kiislamu ilithibitisha kwamba kamwe haitalegeza kamba katika kulinda ardhi yake.