Oct 08, 2024 06:12 UTC
  • Araghchi: Iran itajibu vikali chokochoko zozote za utawala wa Kizayuni

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa Tehran haina nia ya kushadidisha mivutano wala kuzusha vita katika eneo hili lakini wakati huo huo iko imara na tayari kutoa majibu makali zaidi iwapo utawala wa Kizayuni utafanya chokochoko zozote dhidi yake.

Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo wakati alipozungumza kwa njia ya simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Misri, Badr Abdelatty ambapo pande mbili zimetilia mkazo udharura wa kuongezwa jitihada za kidiplomasia za kukomesha jinai na mashambulizi ya Israel huko Lebanon na Ghaza na kupelekwa haraka misaada ya kibinadamu kwa watu wa maeneo hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia ziara yake ya hivi karibuni ya kuutembelea mji mkuu wa Lebanon, Beirut na hali ya Muqawama wa nchi hiyo na kusema kuwa, Muqawama wa wananchi wa Lebanon ni wa kupigiwa mfano na kwamba, wanamapambano wa Kiislamu wamejiandaa vilivyo kukabiliana na uvamizi wa aina yoyote ile wa nchi kavu wa jeshi dhalimu na Israel. 

Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

 

Vilevile amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaki kuona kunazuka vita vikubwa katika eneo hili kama ambavyo haina nia kabisa ya kushadidisha mgogoro, lakini wakati huo huo imejiandaa kikamilifu kutoa majibu makali kwa utawala wa Kizayuni iwapo utawala huo vamizi utafanya uchokozi mwingine wowote dhidi ya Iran.

Baada ya kuvumilia kwa muda wa kutosha, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumanne ya wiki iliyopita ililazimika kuutia adabu utawala wa Kizayuni baada ya dola hilo pandikizi kufanya jinai zisizovumilika tena. 

Makombora ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH yalitwanga vikali maeneo muhimu na nyeti ya kijeshi na kiusalama ya utawala wa Kizayuni ambapo asilimia 90 ya makombora ya Iran yalipiga kwa ustadi wa hali ya juu maeneo hayo ya Israel.