Mchango wa wazi wa Marekani katika mauaji ya kimbari ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i117268
Mwaka mmoja umepita tangu yalipoanza mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza. Sababu muhimu ya kuendelea kushuhudiwa mauaji hayo ya kimbari na vilevile vita dhidi ya Lebanon katika mwezi uliopita ni uungaji mkono wa kila upande wa Marekani kwa utawala vamizi wa Israel.
(last modified 2024-10-08T07:44:05+00:00 )
Oct 08, 2024 07:44 UTC
  • Mchango wa wazi wa Marekani katika mauaji ya kimbari ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Gaza

Mwaka mmoja umepita tangu yalipoanza mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza. Sababu muhimu ya kuendelea kushuhudiwa mauaji hayo ya kimbari na vilevile vita dhidi ya Lebanon katika mwezi uliopita ni uungaji mkono wa kila upande wa Marekani kwa utawala vamizi wa Israel.

Jumatatu ya jana 7 Oktoba ilisadifiana na kutimia mwaka mmoja tangu kutekelezwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqswa.

Baada ya Operesheni ya Kimbunga ya Al-Aqsa, utawala wa Kizayuni ulianzisha mauaji ya halaiki huko Gaza kwa kisingizio cha hatua halali ya kujihami. Hii ni katika hali ambayo, viongozi mbalimbali wametangaza mara kwa mara kwamba, kile ambacho utawala wa Kizayuni wa Israel unakifanya dhidi ya Gaza si hatua halali ya kujihami, bali ni ukandamizaji na utumiaji nguvu kupita kiasi ambao umesababisha mauaji ya kimbari huko Gaza na jinai dhidi ya binadamu.

Kuna sababu mbalimbali zinazowaandalia mazingira Wazayuni ya kufanya jinai kubwa dhidi ya Gaza na vile vile kuanza vita dhidi ya Lebanon na njama za kuifanya Lebanon iwe Gaza nyingine. Hata hivyo, moja ya sababu muhimu zaidi ni kuhusiana na uungaji mkono wa kila upande wa Marekani kwa jinai za utawala huo ghasibu unaofanya mauaji ya kikatili hata dhidi ya watoto wachanga na wagonjwa hospitalini.

Historia inaonyesha kuwa, utawala dhalimu wa Israel ni mpokeaji mkubwa zaidi wa misaada ya kijeshi ya Marekani na tangu 1959 hadi sasa imepokea dola bilioni 251.12, kwa kuzingatia kiwango cha mfumuko wa bei katika miaka hii.

Pamoja na hayo, dola bilioni 17.9 zilizotumika tangu Oktoba 7 mwaka jana (2023) ni misaada mingi zaidi ya kijeshi iliyotumwa kwa Israel katika mwaka mmoja uliopita. Misaada ya Marekani tangu kuanza kwa vita vya Gaza imejumuisha ufadhili wa kijeshi, uuzaji wa silaha, utoaji wa vifaa na kadhalika.

 

Kwa mujibu wa gazeti la Times of Israel na kwa mujibu wa ripoti hii, silaha nyingi zilizotolewa na Marekani katika kkipindi cha mwaka huu mmoja zilijumuisha kuanzia risasi za mizinga mpaka makombora ya mizinga na mabomu ya pauni 2,000 pamoja na mabomu ya kuongozwa yenye umakini.

Mbali na misaada ya kijeshi na kifedha ya Marekani kwa utawala wa Kizayuni, Washington pia imeuunga mkono hadharani utawala wa Kizayuni katika majukwaa ya kimataifa na kuzuia kupitishwa azimio lolote la kusimamisha vita dhidi ya Gaza. Kwa kutumia haki ya kura ya turufu katika Baraza la Usalama, Marekani sio tu kwamba haikuruhusu kupasishwa azimio lolote dhidi ya utawala wa Kizayuni, bali pia ilidai kuwa, kinachofanywa na utawala huo wa Kizayuni ni kujilinda na kujihami na kwamba, hatua hiyo ni halali.

Hii ni katika hali ambayo, dai hili la Marekani linapingwa vikali na fikra za umma duniani na hata ndani ya Marekani kwenyewe na ushahhidi wa wazi wa hilo ni kufanyika kwa maandamano makubwa ya wanafunzi, maprofesa na watu wanaokosoa sera za Marekani na kuunga mkono Palestina. Katika kumbukumbu ya mwaka mmoja wa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa hapo jana na katika mkesha wa siku hiyo, miji mbalimbali ya Marekani ilishuhudia maandamano makubwa ya kuunga mkono Palestina.

 

Tukiachana na misaada ya moja kwa moja ya Marekani ya kifedha, kijeshi, kisiasa na vyombo vya habari kwa Israel, Washington ikiwa na lengo la kuiunga mkono Israel imeliweka katika ajenda zake suala la kuchukua hatua hasi, kama vile kuweka vikwazo dhidi ya nchi nyingine na kupitisha sheria za kuzuia kudhoofishwa Israel.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Abdul-Malik al-Houthi, Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen akasema katikka hotuba yake kwenye kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kutekelezwa Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqswa kwamba: Marekani na nchi za Magharibi ni waitifaki, washirika na wafadhili wa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na zinashiriki katika mauaji na maafa dhidi ya taifa la Palestina.

Kiongozi huyo wa Ansarullah amebainisha kwamba, adui Israel ametekeleza zaidi ya mashambuli ya anga 250,000 na ya mizinga dhidi ya Ukanda wa Gaza katika mwaka uliopita, na kutumia tani 100 za mada za milipuko mbali na mabomu, roketi na risasi kuwaua Wapalestina, ambapo sehemu kubwa ya zana hizo za vita zimetolewa na serikali ya Marekani.