US yaweka rekodi mpya ya kuogofya, yatimua maelfu ya watoto
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128344
Zaidi ya watoto 8,300 wahamiaji wasio na vibali, wenye chini ya umri wa miaka 11 walipewa maagizo ya kufukuzwa nchini Marekani mwezi Aprili, hiyo ikiwa ni idadi ya juu zaidi ya kila mwezi kuwahi kurekodiwa nchini humo.
(last modified 2025-07-15T06:22:36+00:00 )
Jul 15, 2025 04:43 UTC
  • US yaweka rekodi mpya ya kuogofya, yatimua maelfu ya watoto

Zaidi ya watoto 8,300 wahamiaji wasio na vibali, wenye chini ya umri wa miaka 11 walipewa maagizo ya kufukuzwa nchini Marekani mwezi Aprili, hiyo ikiwa ni idadi ya juu zaidi ya kila mwezi kuwahi kurekodiwa nchini humo.

Gazeti la The Independent limeripoti hayo likinukuu data za mahakama na kueleza kuwa, aghalabu ya watoto hao wanawajihiwa na majaji wa uhamiaji wakiwa peke yao, bila mawakili au walezi.

Rais wa Marekani, Donald Trump amepasisha sera kandamizi za uhamiaji tangu kurejea kwake madarakani, akimshutumu mtangulizi wake Joe Biden kwa kuwezesha eti uhamiaji haramu mkubwa.

Tangu kuapishwa kwa Trump mnamo Januari mwaka huu, majaji wa uhamiaji wameripotiwa kuamuru kufukuzwa nchini Marekani zaidi ya watoto 53,000, wengi wao wakiwa katika shule za msingi au chekechea.

Baadhi ya watoto hao wahamiaji wanaripotiwa kutokuwa na walezi nchini Marekani, huku mamlaka za uhamiaji zikiacha kufuatilia tena kesi kama hizo.

Wanasheria wameiambia The Independent kwamba, watoto hao mara nyingi hawaelewi mchakato wa kisheria wanapokabiliwa na kesi za kufurushwa nchini Marekani.

Katika kisa kimoja, mtoto wa miaka sita aliripotiwa kutenganishwa na babake, akazuiliwa kwa miezi minne, na kufukuzwa nchini Marekani bila ya msaada wa kisheria baada ya ufadhili wa serikali kukatwa.