Iran: Mauaji ya kigaidi ya Jenerali Soleimani yalikiuka Hati ya UN
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i62112-iran_mauaji_ya_kigaidi_ya_jenerali_soleimani_yalikiuka_hati_ya_un
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mauaji ya kioga na kigaidi ya aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Luteni Jenerali Qassem Soleimani yaliyofanywa na jeshi katili la Marekani mapema mwaka huu nchini Iraq ni ukiukaji wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 10, 2020 07:33 UTC
  • Iran: Mauaji ya kigaidi ya Jenerali Soleimani yalikiuka Hati ya UN

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mauaji ya kioga na kigaidi ya aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Luteni Jenerali Qassem Soleimani yaliyofanywa na jeshi katili la Marekani mapema mwaka huu nchini Iraq ni ukiukaji wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa.

Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kubainisha kuwa, "mauaji ya kioga ya Jenerali Soleimani-shujaa wa kupambana na ugaidi katika eneo, yalikuwa mauaji ya kiholela na ukiukaji wa wazi wa Hati ya UN. Marekani inabeba dhima ya jinai hiyo na wala haiwezi kulifuta hili kwa kuibeza UN."

Amesema katu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasahau wala kusamehe ugaidi huo wa kiserikali uliofanywa na Washington.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hayo katika hali ambayo, kikao cha 44 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva hapo jana kililaani vikali jinai zinazofanywa na serikali mbali mbali duniani, yakiwemo mauaji ya kigaidi ya Shahidi Soleimani.

Wiki iliyopita, Mwendesha Mashtaka wa Tehran alitoa waranti wa kutiwa mbaroni watu 36 akiwemo Rais Donald Trump wa Marekani wakihusishwa na mauaji ya Shahid Qassem Soleimani. Mwendesha Mashtaka wa Tehran alieleza kuwa, tayari wameitaka Polisi ya Kimataifa Interpol kuwatia mbaroni wahalifu hao.

Gari lililokuwa limembeba Soleimani baada ya kushambuliwa na droni ya US

Itakumbukwa kuwa, tarehe 3 Januari mwaka huu, jeshi la kigaidi la Marekani kwa amri ya rais wa nchi hiyo Donald Trump lilimuua kidhulma Luteni Jenerali Qassem Soleimani akiwa uraiani nchini Iraq tena akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Baghdad. 

Nchi nyingi duniani, mashirika, taasisi na makundi mbalimbali yalilaani vikali mauaji hayo ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani dhidi ya kamanda huyo shujaa aliyekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya magenge ya kigaidi katika eneo la Asia Magharibi.