Iran: Mauaji ya Soleimani ni mfano wa wazi wa ugaidi wa kiserikali
Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu katika Umoja wa Mataifa amesema mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na jeshi la Marekani dhidi ya aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Luteni Jenerali Qassem Soleimani akiwa ugenini nchini Iraq ni mfano wa wazi wa ugaidi wa kiserikali.
Majid Takht-Ravanchi amesema hayo katika Mkutano wa Wiki ya Kupambana na Ugaidi uliofanyika kwa njia ya intaneti na kuongeza kuwa, mauaji hayo ya Shahidi Soleimani ni kielelezo cha wazi cha ukiukaji wa sheria za kimataifa na ugaidi wa kiserikali wa Marekani.
Amesema hatua za upande mmoja zinazochukuliwa na Marekani zinakwamisha jitihada za kimataifa za kupambana na ugaidi. Amebainisha kuwa, Marekani ni muungaji mkono wa kundi la kigaidi la MKO ambalo limeua Wairani zaidi ya 12,000.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza bayana kuwa, Marekani inapaswa kubebeshwa dhima kwa jinai yake hiyo ya kumuua kigaidi Jenerali Soleimani.
Kadhalika Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu katika Umoja wa Mataifa amesema vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa la Iran ni ugaidi wa kiuchumi. Amesema sera ya mashinikizo ya juu ya Marekani inalenga moja kwa moja raia wa kawaida wasio na hatia.
Wakati huohuo, Majid Takht-Ravanchi amesema Marekani inapaswa kubebeshwa dhima kwa mauaji yanayoendelea ya wananchi wa Yemen, kwa kuiuzia silaha Saudia.